Jumanne, Disemba 12, 2017
Desemba 12, 2017.
JUMANNE, JUMA LA 2 LA MAJILIO
Somo la 1: Isa 40:1-11 Isaya wafariji watu wangu kwamba Mungu mwenyewe atakuja kuwaokoa; kama mchungaji atawalisha na kuwachukuwa kondooo wake kifuani pake.
Wimbo wa katikati: Zab 95: 1-3, 10-13 unapaza sauti kwamba Mungu wetu anakuja na nguvu.
Injili: Mt 18: 12-14 mfano wa kondoo aliyepotea unatueleza jinsi Mungu anavyo mshughulikia kila mmoja wetu ambaye anaenda njee na malisho yake.
.
MUNGU ANATAFUTA KONDOO ALIYEPOTEA!
Somo la kwanza kutoka katika kitabu cha nabii Isaya, tunasikia sifa za Mchungaji mwema mwenye huruma na kuwajali kondoo waliopotea (watu wa Israeli). Katika Injili Yesu anatupa mfano wa kondoo aliyepotea. Huyu Mchungaji anawaacha wale tisini na tisa na kwenda kumtafuta aliyepotea. Mfano huu unaendelea na kusema kuwa “atakapo mpata, Amin, nawaambia, atafurahi zaidi juu ya kondoo huyu, kuliko wale tisini na tisa ambao hawakupotea” (Mt 18:13). Huzuni na masikitiko ya huyu Mchungaji yanabadilika na kuwa furaha baada ya kumpata kondoo na kumrudisha kwenye kundi. Kwa haraka haraka inawezekana kuonekana kama sio sawa kwa Mchungaji kumfurahia zaidi huyu aliyepotea baada ya kumpata kuliko wale tisini na tisa. Lakini tukitambua kwamba, kila mmoja wetu ni yule kondoo aliyepotea, ina leta maana zaidi. Tunapotafakari kuhusu mfano huu ni vizuri kufikiria juu ya hamu na tamaa ya huyu Mchungaji na jitihada zake za kututafuta. Hii ndio hali ya Mungu juu yetu. Mungu anatutafuta daima aturudishe kundini mwake.
Mungu kutuhangaikia na kututafuta haina maana anahitaji kitu kutoka kwetu, lakini anahitaji yote kutoka kwetu. Kujikabidhi kwake kuna maana kwamba tunatambua kwamba kila kitu chema kimetoka kwake pamoja na sisi wenyewe. Pili anahitaji kuturudishia kila kitu, kikiwa kimebarikiwa na kutakaswa. Inaweza kuwa vigumu kutambua kwamba sisi sote tunamtegemea Mungu. Hakuanzisha ubinadamu ili atufanye watumwa. Bali kutupatia uhuru. Tunaweza kutumia uhuru huo na kuanza kushanga shangaa na kupotea, lakini pia kuna furaha zaidi tunapo patikana tena. Mchungaji mwema anatuchukulia kwa umuhimu sana na daima bila kusita anakuwa nasi na kutufuata hata kwenye hatari, kwenye makorongo, kutuficha mahali mpaka mbwa mwitu wapite.
Tutafakari leo, kuhusu wewe kuwa mmoja wa yule kondoo aliyepotea. Kupotelea kwenye “dhambi” sio jambo linaloleta furaha, dhambi inaleta wasi wasi, maumivu, kukosa Amani, kuchanganyikiwa, hasira na mengine mengi. Lakini tukiinua macho yetu kumwelekea Mchungaji mwema tukiwa katika hali ya dhambi zetu, tutapata tena matumaini mapya. Tutapata matumaini kwamba Mungu wetu anatujali na hachoki kamwe kututafuta. Na anapo tupata moyo wake hujazwa na furaha kuu! Wakati kondoo aliyepotea anapopatikana jumuiya yote ya mbinguni hufurahi. (Lk 15:7).
Sala:
Bwana, katikati ya dhambi zangu na kuchanganyikiwa nakurudia. Nina amini kwamba unanitafuta. Ninaomba nijiaminishe kwenye upendo wako wa hali ya juu kwangu. Yesu, nakuamini wewe.
Amina
Maoni
Ingia utoe maoni