Jumamosi. 23 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatano, Oktoba 04, 2023

Jumatano, Oktoba 4, 2023
Juma la 26 la Mwaka

Kumbukumbu ya Mt. Fransisko wa Assis

Neh 2: 1-8;
Zab 136: 1-6;
Lk 9: 57-62


GHARAMA YA KUWA MFUASI WA KRISTO!

Tunaishi katika ulimwengu ambao gharama za maisha zinapanda kadiri ya mahitaji yanavyopanda. Na wakati mwingine kadiri gharama inavyopanda ndivyo tunavyo hitaji zaidi. Kuna gharama ya kumfuata Kristo pia! Katika Injili, watu watatu wanakuja kwa Yesu na wanataka kumfuata. Lakini Yesu alivyo ongea kuhusu gharama ya kumfuata hawakuwa tayari kuilipa. Walitaka kuwa na Yesu lakini katika hali yao wenyewe. Hawakuwa tayari kuachia mambo yao, tamaa zao, mipango yao n.k, kwa ajili ya Kristo.

Haishangazi kwani hata Yesu alisema njia ya kwenda kwenye uzima wa milele ni nyembamba na ni wachache watakao ipata. Nehemia alikuwa mbeba kikombe katika mahakama ya Mfalme Artaxerxes. Mbeba kikombe alikuwa ni mtu mwenye madaraka makubwa katika mahakama, ambaye kazi yake kubwa ilikuwa pia kuhudumia vinywaji katika meza ya kifalme. Mtu mwenye hofu na mabaya, na mwenye kuhesabiwa adabu njema ndiye pekee aliyeweza kupewa mamlaka haya. Alikuwa na kazi ya kulinda kikombe cha mfalme asije akawekewa sumu, na alikuwa lazima anywe divai kidogo mbele ya watu kabla haja anza kuhudumia watu. Nehemia, ambaye ni mgeni katika nchi ya kigeni, alionekana mtu mwenye kuaminika. Kwa kutambua kwamba kuta za Yerusalem zilikuwa zimebomoka alimwuomba ruhusa Mfalme aende kuzijenga. Artaxerxes alimtuma kama gavana wa Yuda ili aende kuzijenga kuta hizo. Akiwa huko, aliwapa changamoto kwa kuwapinga maadui wa Yuda pande zote-Wasamaria, Waamori, Waarabu na Wafilisti na akajenga kuta hizo kwa muda wa siku 52. Kinacho tugusa sisi ni upendo wa Nehemia kwa mji wa Yerusalem, mji Mtakatifu, ambao pia ulikuwa na hekalu-nyumba ya Mungu. Je, ni upendo gani tulionao juu ya nyumba ya Mungu na utume wa Bwana? Je, tumejitoa kiasi ambacho tunaweza kuweka maisha yetu katika hatari?

Wito wa Yesu. Anapo tuita sisi tunapaswa kuitika kwa moyo wote na kujitoa kabisa kwa moyo wetu wote na kwa ukarimu wote. Katika somo la Injili, Bwana alitamani yule mtu wa tatu mara moja angemfuata mara moja. Lakini huyu mtu anageuka nyuma anataka aende kwanza kwenda kuwaaga kwanza nyumbani. Lakini Yesu anaweka wazi kwamba yeyote yule anayeitwa anapaswa kuitika mara moja na kumfuata. Yesu anatumia wakati huu kutukumbusha kwamba utume wetu wa kwanza ni kuitika na kwenda kufanya kazi yake. Katika wito wetu wa kumfuata Kristo, tunapaswa kuwa tayari kumfuata Kristo, tunapaswa tuitike bila kuangalia angalia nyuma. Katika maisha yetu wenyewe, tunaweza tusipate ule wito wa kuacha kila kitu katika hali ya kuacha vyote na kuondoka kumtumikia Kristo katika hali nyingine ya maisha. Lakini hapa cha muhimu ni utayari wetu na majitoleo yetu juu ya nyumba ya Mungu.

Katika siku hii tunapo mkumbuka Mt. Fransisko wa Assis yeye alimfuata Yesu bila kujibakiza kwa kuacha mali na anasa mbali mbali na hivyo kumfuata Kristo mwenyewe katika hali ya ukaribu kabisa. Yeye aliipenda nyumba ya Mungu, ambayo katika maono aliambiwa akaijenge kwani inabomoka. Kwa maisha yake aliwavuta wengi mno kwa Kristo na ndio maana hata siku hizi yapo mashirika mengi sana yanayo fuata karama yake. Tuwaombee Wafransisko wote waendelee kumtangaza Kristo kwa maisha yao.

Sala:
Bwana, ninakupenda wewe na ninataka kukufuata wewe. Nisaidie mimi niweze kushinda kitu chochote kinacho weza kunirudisha nyuma nishindwe kusema “ndiyo” kwa wito wa kutimiza mapenzi yako matakatifu. Yesu nakuamini wewe.
Amina.

Maoni


Ingia utoe maoni