Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatatu, Machi 21, 2022

March 21 2022.

JUMATATU, JUMA LA 3 LA KWARESIMA

KUINGIA KATIKA MAPENDO NA YESU!
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Leo neno la Bwana tutaanza kwa kuliangalia somo la kwanza ambapo tunasikia juu ya kuponywa kwa mkoma aitwaye Naamani. Mkoma huyu aliponywa tu baada ya kuwa mnyenyekevu, baada ya kusikiliza kile Mungu anachosema, baada ya kusikiliza kile nabii anachosema. Hiki ndicho kilichokuwa sababu ya Baraka kwake.
Tumesikia kwamba kutii kulimwia vigumu kwani aliambiwa kitu ambacho machoni pa wengi kilionekana kama kinamshusha hadhi, yeye mwenyewe na taifa lake, kwamba maji ya mito ya nchini mwake sio bora kuliko ya Israeli. Yeye alipoambiwa akajichovye kwenye hiyo mito alikasirika. Lakini alipokubali mambo yalimwia vizuri.
Hili ni fundisho kubwa kwetu ndugu zangu kwamba endapo nasi tutakuwa tayari kuisikiliza sauti ya Bwana, basi hili litakuwa chanzo cha Baraka kwetu. Mara nyingi tumemzuia Bwana kufanya kazi kwa sababu tumeshampangia Bwana tayari utaratibu wa namna anavyopaswa kufanya kazi. Hili limetuletea wengi kati yetu madhara makubwa.
Katika injili, Yesu anasifu tukio la Naamani na anaongezea tena na tukio la mama mjane wa Serepta. Wote wawili walikuwa tayari kuachana na mipango ya vichwa vyao na kumwacha Mungu afanye kazi na nakwambia kama wote wangekataa kumsikiliza Mungu na kufuata mipango ya vichwa vyao, hakika wangeangamia-Naamani angeangamizwa kwa ukoma wake na mama mjane wa Serepta angeangamizwa na njaa na kufa.
Hili ni fundisho kwetu. Pale tutakapofungua milango kwa ajili ya Bwana hakika Bwana atafanya kitu na kuja kati yetu na kutubariki zaidi na zaidi. Tumsifu Yesu Kristo.

Maoni


Ingia utoe maoni