Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatano, Februari 23, 2022

Jumatano, Februari 23, 2022,
Juma la 7 la Mwaka wa Kanisa
Mk 9: 38-41.

Karibuni ndugu zangu wapendwa kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo neno la Bwana katika zaburi ya wimbo wa katikati inatueleza kwamba wale waipendao sheria yako ee Bwana wana amani tele. Amani huanza kwa kuyapenda mambo ya Mungu, heshima tunayoipatia vitu vitakatifu na vipaumbele tuvitoavyo kwavyo hakika hutupatia amani tele.
Sisi tuyapende matakatifu, haya ndiyo yatakayo tupatia hekima. Tuwe makini na picha na habari tunazosikiliza. Wengi wamepoteza hekima na amani ya moyoni mwao kwa sababu ya kuangalia picha mbaya na kusikiliza umbea au yasiyofaa. Mwishowe wameshindwa kutambua lililojema maishani mwao na kuwa maskini na kuthamini maisha ya uzembe. Sisi tupendelee matakatifu na hakika tutajipatia huko hekima. Tuchangie pia kwa maendeleo ya kanisa na hakika tutajipatia hekima.
Kwenye somo la injili, tunakutana na muumini mwenye kutoa pepo kwa kutumia jina la Yesu. Huyu muumni alitambua kwamba Yesu ndiye njia, ukweli na uzima na hakika hakuna awezaye kuja kwa Baba isipokuwa kwa kupitia Yeye.
Watatokea wengi na wataomba kwa jina la Yesu watapata pengine zaidi kuliko sisi. Wengine watafanya mambo makubwa kuliko hata sisi kwa sababu ya kumheshimu Yesu huyu huyu, kwa sababu ya kutambua kwamba Yesu ndiye njia, ukweli na uzima. Sisi tujifunze kushirikiana nao tupate kuukuza ufalme wa mbinguni, tumfanye Yesu atukuzwe zaidi maishani mwa mwanadamu.
Isije ikafika mahali tukadhani neema ni kwetu tu ambao tumetangulia kumfahamu Yesu. Wapo ambao waweza kumfahamu kwakuchelewa lakini imani yao ikawa kubwa kuliko ya kwetu tuliotangulia, tukiona hivyo tusione wivu na kuanza kuwazuia au kuwawekea vikwazo, tuungane nao tujenge pamoja Utawa wa Yesu.
Somo hili pia litusaidie kubadilisha mtazamo wakudhani kuwa kuna familia maalumu za kutoa makuhani tuu na watawa nakudhani kwamba familia nyingine haziwezi. Familia zile zinazojitahidi kuchipusha miito tuwatie moyo tusiwazuie nakudhani ukoo au familia fulani ndio wanao stahili tu.

Maoni


Ingia utoe maoni