Jumamosi, Januari 08, 2022
Jumamosi, Januari 8, 2022,
1 Yoh 5:14-21;
Zab 149: 1-6.9;
Yn 3:22-30.
KUBAKI DAIMA KWAKULITAZAMA FUMBO LA NOELI
Karibuni sana wapenzi wa Bwana kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana katika somo la injili, Yohane anafurahi pale asikiapo kwamba Yesu ameanza kubatiza. Anafurahi kwa sababu anajua kwamba huo ndio ubatizo mkuu kuliko ubatizo uliofanywa na yeye.
Yesu ameleta ubatizo wa moto na ubatizo wa Roho. Ubatizo wa namna hii unapaswa umfikie kila mmoja, upate kuleta upatanisho kamili kati ya Mungu na mwanadamu na kufungua mbingu ambayo ilifungwa kwa kosa la wazazi wetu wa Mwanzo, Adamu na Eva. Yohane anakuwa tayari kupisha njia ili ubatizo wa namna hii upate kuifikia dunia, uiletee furaja na furaha na urafiki na Mungu.
Sisi tujifunze toka kwa Yohane. Tujiangalie sisi wenyewe kama utendaji wetu unafanania na ule wa Yohane; isije ikawa uwepo wangu mahali fulani unazuia eneo hilo kupata maendeleo zaidi. Wapo viongozi walioongoza eneo moja kwa muda mrefu, muda wote wapo tu pale, lazima ifike mahali wajiulize, je, uwepo wangu katika jumuiya hii au nafasi yangu imeleta mabadiliko au nimezuia watu wa Mungu kufaidi zaidi? Tuwe tayari kuachia madaraka, tuwaachie wenzetu, wapo walio wazuri zaidi-tusifikirie kwamba sisi ndio kila kitu, ati tukiondoka, basi hakuna kitakachofanyika.
Katika kanisa, upo uhamisho wa watu mbalimbali, hata kama ni wazuri kiasi gani, watahamishwa tu ili wasije wakangangania eneo moja na kusababisha ubatizo wa moto na wa roho kutokea. Tuondokane na dhana ya namna hii. Hivyo, leo tujiulize ni wapi inabidi tufanye kama Yohane-kuna watu ambao tangu nikiwa mdogo bado ni viongozi kanisani-wanangangania madaraka yale yale, lazima ifike mahali wajiulize, je, uwepo wao unaleta baraka zaidi au wanazuia ubatizo wa moto usiwapate waamini? Yohane hakuwa tayari kuzuia ubatizo wa Moto na wa Roho. Nawe usizuie ubatizo huu.
Katika somo la kwanza, Yohane anaendelea kutupatia mawaidha mazuri sana kwamba Yesu ndiye uzima wa milele. Tukikaa ndani yake twaokolewa na dhambi zote, hata dhambi ya mauti haitapata mamlaka juu yetu. Na pale tutakapoomba kwa mapenzi yake, tutapokea tuombalo. Sisi tusiache kumwelekea Bwana Yesu. Yeye ndiye uzima wetu. Hivyo, tuzidi kumwamini na kumkabidhi maisha yetu yote.
Maoni
Ingia utoe maoni