Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatatu, Januari 10, 2022

Jumatatu, Januari 10, 2022
Juma la 1 la Mwaka.

1Sam. 1:1-8
Zab. 116:12-14, 17-19 (K)
Mk. 1:14-20

KUISIKILIZA SAUTI YA MUNGU!
Karibuni sana wapendwa wa Bwana kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana katika somo la injili, Bwana Yesu anaanza utume wake hadharani. Hii ni baada ya Yohane kutiwa Gerezani.
Sijui Yohane alijisikia vipi, yaani baada ya kufanya kazi yote kubwa hii, baada ya kumbatiza Yesu na kumtambulisha machoni pa wote, Yohane anaishia gerezani. Inaonekana kwamba Yohane kama Nabii aliendelea kumtumainia Mwenyezi Mungu. Lakini ndivyo hali ilivyo, mara nyingi, mtu mwema ndiye anayedhulumiwa kuliko alivyo mwovu. Hata mti mzuri hutupiwa mawe mengi zaidi kuliko ilivyo miti mingine mibaya kama vile miiba.
Sisi tuwe tayari kuvumilia pale tunapomfuata Bwana. Yesu anapoanza utume wake, ujumbe anaoanza nao ni wa kutubu na kuiamini injili. Huu ndio utakaoiokoa dunia. Duniani dhambi nyingi zinatendeka na madhara ya dhambi ya mmoja huwafikia wengi kwani duniani tunaishia kwenye jamii na kosa la mmoja huiadhiri dunia nzima. Hivyo, tunapaswa kuomba msamaha hata kwa ajili ya makosa yasiyotendwa na sisi.
Yesu anapoendela na utume wake, anawaita wafuasi wake na kuwaahidi kuwa wavuvi wa watu zaidi kuliko wa samaki. Mwanadamu ni kiumbe kikuu kuliko viumbe vingine. Hivyo, kuwa mvuvi wake ni miongoni mwa heshima kubwa mwanadamu anaweza kupewa. Hii yaashiria kwamba lengo la Yesu ni kutukabidhi vitu vyema.
Sisi ndio wenye kujichagulia vitu visivyo na thamani na kudhania kwamba ni vyenye thamani. Tujifunze kutafuta yaliyo ya thamani toka kwa Bwana. Tunyanyuke na kumfuata Yesu nasi tutaonyeshwa ya thamani. Tutatumia muda wetu kwa ajili ya thamani. Tutafanya ya thamani na kujifunza ya thamani.
Katika somo la kwanza, Hanna, atakayekuja kuwa mama yake Samweli, anaonekana kudharaulika machoni pa Penina, aliye mke mwenza. Hanna ataendelea kumlilia Mungu na Mungu atampatia mtoto, tena atakayekuja kuisaidia Israeli kwa muda mrefu sana. Hakika Mungu ana mipango yake. Na pale anapoichelewesha, jua kwamba kuna mambo mazuri anataka yatokee na mambo mazuri hayahitaji haraka.
Mwanadamu anapaswa kuwa mvumilivu pale anaposubiri haya yaliyo mazuri. Asiwe na moyo wa papara na Bwana kwa hakika atamsaidia tu. Uvumilivu ni mlango wa kutufungulia kuyapata yaliyo makubwa na mazuri zaidi. Tuombe kuwa wavumilivu.

Maoni


Ingia utoe maoni