Jumatano, Disemba 29, 2021
Desemba 29, 2021.
------------------------------------------------
JUMATANO, OKTAVA YA NOELI
Somo la 1: 1Yn 2: 3-11 Yohane anatuambia kwamba hatuwezi kumfahamu Yesu hadi tumeshika amri zake: kumpenda Mungu na jirani.
Wimbo wa katikati: Zab 95: 1-3,5-6 Mwimbieni Bwana wimbo mpya, tangazeni wokovu wake siku kwa siku na maajabu yake kati ya watu.
Injili: Lk 2: 22-35 Luka anatuambia kuhusu kutolewa kwa mtoto Yesu hekaluni, na Simeon anatabiri kwamba upanga utapenya katika moyo wa Maria Mama yake Yesu.
------------------------------------------------
UWEPO WA MUNGU KATI YETU!
Liturjia ya leo inatabiri kuhusu wakati uliopita lakini pia inatabiri muda mfupi ujao. Ni siku chache tu zilizopita tumesheherekea kuzaliwa kwa Yesu, na furaha ya sikukuu hii haiwezi kuisha. Katika somo la Injili tunamuona Simeoni nabii. Mtu huyu Mtakatifu alikuwa ameandaliwa na Mungu kwa ufunuo wake mwenyewe kwamba angemuona Masiha kwa macho yake, mkombozi wa ulimwengu. Siku zote za maisha yake amekuwa akitarajia hili. Alitamani na kusubiri kwa siku hii. Pale tu Maria na Yosefu walipo mpeleka mtoto Yesu hekaluni Simeoni alitambua ndani ya moyo wake kwamba mtoto huyu ndiye Mkombozi tuliye ahaidiwa. Maneno yake yana nguvu. Anasema “Bwana waweza kumruhusu mtumishi wako aende kwa Amani..kwa macho yangu nimeuona wokovu utokao kwako..” Simeoni alitambua kwamba maisha yake sasa yalikamilika. Alikuwa tayari sasa kufa kwani alipewa upendeleo wa kumuona Kristo. Alimshika mikononi mwake akampa Mungu utukufu kwa wakati ule.
Mtoto aliyeshikwa na Simeoni ni Mungu kweli kweli. Lakini alikuwa Mungu katika mwili wa mtoto mdogo. Simoni hakika alimuona kwa jinsi alivyokuwa na kufurahi. Tunapaswa kutambua uwepo wa Masiha na kuufurahia kama Simeoni. Yesu yupo hai kwa kila moyo tunaopewa na Mungu, katika kila sakramenti ya kanisa, kwa kila somo la Maandiko matakatifu, na yupo ndani ya mioyo yetu. Mioyo yetu inapaswa kuwa hilo hekalu ambalo tunatambua uwepo wa Kristo ndani yake na tunapaswa kufurahi kwa kuwa karibu nasi namna hii.
Leo antifona ya wimbo wa kwanza inatupa sababu yote-Mungu mwana asingefanyika mwili hata kidogo kama isingekuwa ni upendo wa Mungu Baba kwetu sisi. “Mungu aliupenda ulimwengu hivi hata akamtoa Mwanae ili wote wanao mwamini wasipotee bali wawe na uzima wa milele”. Jukumu letu ni kukubali ujumbe huu na upendo unaojengeka ndani yake. Kama kuna mtu ambaye alitambua jinsi ya kupokea zawadi hii ni Maria, na Simeoni pia. Maria alikuwa ni wa kwanza wa kupokea zawadi ya Mungu, na akajibu kwa upendo na kujiamini na kujikabidhi kwake. Simoni alimpokea mtoto mikonini mwake akamshukuru Mungu…Macho yangu yameuona wokovu ulioandaa kwa watu wote waweze kuuona.
Sala:
Bwana, ninakushukuru kwa zawadi ya Mwanao ulimwenguni. Tunaomba tupokee zawadi hii kwa mioyo yetu yote. Yesu nakuamini wewe.
Amina
Maoni
Ingia utoe maoni