Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Alhamisi, Disemba 23, 2021

Alhamisi, Desemba 23, 2021,
Juma la 4 la Majilio

Mal 3: 1-4, 23-24;
Zab 24: 4-5, 8-10, 14;
Lk 1: 57-66


KURUDI KWA BWANA!
Ama kweli Yesu ni mkuu. Nabii Malaki katika somo la kwanza anatabiri ujio wa mjumbe kuandaa siku ya ujio wake. Inaonesha kwamba dunia ilijiandaa kwa ujio mkubwa; ujio wa Mungu duniani. Hivyo, iliwabidi watu watubu na kujitakasa ili waupatie heshima uwepo wa Mungu duniani. Dhambi humkufuru Mungu.
Nabii Malaki anatangaza ujio wa mjumbe, Elia kuandaa ujio huo. Sasa katika injili, mjumbe huyu anazaliwa, na Malaika Gabrieli alimweleza Zakaria kwamba Roho na nguvu ya Elia itakuwa juu yake (Lk 1:17). Huyu ndiye atakayewaandaa watu kwa ujio wa Masiha. Yohane alifanya kazi hii kwa uaminifu. Alihubiri na kuwahimiza watu waache dhambi na kubatizwa ubatizo wa toba. Pia alimtambulisha Masiha alipofika. Lakini baadhi walikataa kutubu na kumpokea kama Masiha. Lakini Yesu alivumilia kukaa nao, akavumilia kufuru walizomfanyia. Kweli Yesu alikuwa na huruma sana. Sisi tusiwe kama hawa. Tunapokaribia kuadhimisha kumbukumbu ya kuzaliwa kwake, tumpatie Kristo heshima yake kwa kuziungama dhambi zetu. Pia tuepuke kupokea Ekaristi katika hali ya dhambi.
Tukisha ungama anataka tubaki naye katika hali ya usafi. Yesu aliwaambia wanafunzi wake “Salini msije mkaingia katika vishawishi” (Lk 22: 46). Kwa namna nyingine Sala inamsaidia Mkristo kutokuingia kwenye dhambi au sala ni silaha ya kujikinga dhidi ya muovu. Tunaweza kujiuliza mbona nina Sali lakini ninaanguka kwenye dhambi daima? Wengi wetu hatusali vizuri. Pengine tunasali ili watu watuone watusifu kwamba tunasali sana, wengine tunasali kwasababu tunaogopa kutengwa na jumuiya, wengine tunasali ili kutishia watu watuogope, wengine tunasali watu watuheshimu, wengine tunasali ili watu wakiniona nasali siku ikitokea wanipe nafasi ya kwanza kwasababu wataona nina Mungu ndani yangu.
Aina hizo za sala, shetani akija atakubeba vizuri kama upepo. Sali kwa Baba katika hali ya ndani ya kweli mpe yeye utukufu na heshima yote irudi kwa kwake, na daima jiunge naye katika hali hii, nakwambia hapa maneno ya Yesu yatafanya kazi kweli “kwamba salini ili msiingie katika vishawishi”, hutarudi tena kwenye dhambi kirahisi. Pekee yetu hatuwezi tunahitaji msaada wa Mungu, tumwombe atupe nguvu ili Mwanae azaliwe katika hali ya neema katika roho zetu.

Maoni


Ingia utoe maoni