Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatatu, Disemba 20, 2021

Jumatatu, Desemba 20, 2021,
Juma la 4 la Majilio

Isa 7: 10-14;
Zab 24: 1-6;
Lk 1: 26-38


MUNGU ANAFANYA VITU VYOTE VIWEZEKANE
Karibuni sana wapendwa wa Bwana kwa tafakari ya neno la Bwana asubuhi ya leo. Neno la Bwana katika somo la kwanza Nabii Isaya anatangaza ishara kuu, ya mtoto atakayezaliwa atakayeitwa jina la Emmanuel, yaani Mungu pamoja nasi. Huyu ndiye atakayemsaidia mfalme Ahazi kupambana na maadui wake, waliokuwa wakimwandama kila upande, huyu Emanuel, Mungu pamoja nasi.
Mwenyezi Mungu anaonesha kwamba kwa hakika pale Ahazi atakapoweza kumleta Mungu kati yao, ndipo amani itakapopatikana kwa ufalme wake. Bwana Yesu alipozaliwa ulimwenguni, malaika walipiga kelelele kwa furaha, wakatangaza utukufu kwa Mungu juu na amani iwepo duniani. Yesu ndiye chanzo cha amani hii, kwani ni Mungu mwenyewe amekuja ulimwenguni. Palipo na Mungu, palipo na Emanuel, Mungu yupo kati yao na hakika patakuwa na amani.
Bikira Maria aliweza kupokea ujumbe wa Malaika kwa sababu alikuwa na Mungu ndani yake. Sisi tujitahidi kuwa na Mungu kati yetu. Hapa ndipo tutakapokuwa na amani kama mfalme Ahazi anapoelezwa leo, kwamba ni Emanuel tu ndiye atakayeweza kumletea amani. Emanueli ni sababu ya sisi kutulia na kuishi kwa raha na furaha zaidi. Emanueli awe sababu ya sisi kuchanua zaidi.
Katika somo la injili, tunasikia habari za malaika Gabrieli kutangaza juu ya kuzaliwa kwake Bwana Yesu. Gabrieli alipokelewa na Maria kwa imani kuu kama mjumbe wa Mungu. Kwa ndio ya Maria, aliweza kuyabariki maisha yake na maisha ya ulimwengu. Sisi tujitafakari na kutambua kwamba mara nyingi maisha yetu tunashindwa kuyaletea baraka na pia kushindwa kuuletea baraka ulimwengu kwa sababu ya kusema hapana kwa mapenzi ya Mungu. Tujifunze kusema ndio kwa mapenzi ya Mungu na hapa ndipo tutakapoweza kuyabariki maisha yetu. Mipango ya Mungu japokuwa yaweza onekana kuwa migumu maishani mwetu kwa hakika ndiyo yatakayoleta amani na urahisi maishani mwetu.
Zaburi ya wimbo wetu wa katikati imetuhimiza kufungua milango ili mfalme wetu, mfalme wa amani apate kuingia. Yesu ndiye mfalme huyu. Tujifunze kusema ndio kwa mapenzi yake kama alivyofanya Mama Maria na kwa hakika tutaweza kubarikiwa na kufurahia zaidi. Tumefunga milango mingi kwa chuki, visasi na kutokusamehe. Tufungue ili mfalme wa amani aingie arudishe tena amani yetu.

Maoni


Ingia utoe maoni