Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumanne, Disemba 14, 2021

Jumanne, Desemba 14, 2021,
Juma la 3 la Majilio

Sef 3: 1-2, 9-13;
Zab 34: 2-3, 6-7, 17-19, 23;
Mt 21: 28-32


JE, WEWE NI MDHAMBI?

Somo la leo kutoka katika kitabu cha nabii Sefania, linatoa onyo na ole kwa wale wanaokataa kusahihishwa, wanaokataa kusikia, na kuitika wito wa kumwamini Mungu. Katika somo la Injili, Yesu anasema kwamba ‘Watoza ushuru na wenye dhambi wataingia katika Ufalme wa Mungu kabla ya viongozi wa dini’. Je, ni kweli kwamba watoza ushuru na wenye dhambi waliingia katika Ufalme wa Mungu kabla ya viongozi wa dini ya Wayahudi? Je, Yesu alikuwa anasema kweli kwamba utakatifu wa watoza ushuru na makahaba ulizidi ule wa viongozi wa dini? Ndio, ilikuwa hivyo kwasababu majivuno yaliwafanya viongozi wa dini kuwa na moyo mgumu wa kupokea ujumbe wa Ufalme wa Mungu alioleta Yesu mwenyewe kwa maneno yake. Walifikiri juu ya ukubwa wao sana na walipenda wengine wawaze juu ya ukubwa wao. Walikuwa wamejiridhisha wenyewe kwa utakatifu wao wenyewe, nakujiona wema kabisa, jambo ambalo ni mbaya kweli. Lakini Yesu anayaona yote hayo, na anawanyanyua watoza ushuru na wenye dhambi kwa utayari wao wakutubu na kumpokea, Yesu anawapandisha kwenye thawabu ya Ufalme wa Mungu.

Tujitafakari sisi wenyewe kama tunamfanano na tabia ya viongozi wa dini wa Wayahudi wa kipindi hicho au tuna tabia ya hawa watoza ushuru na wenye dhambi waliokubali kupokea maneno ya Yesu. Pengine, ni vigumu kukubali. Pengine tumejitengenezea tabia ya kujitambulisha sisi wenyewe kama watu wazuri na wasio na kosa na wenye haki. Yesu anataka tujione wenyewe katika kundi hili la watoza ushuru na wenye dhambi. Hii ni kwasababu sisi wote ni wadhambi. Tunaweza tusiwe katika hali ya kuumia moyoni kama wao walivyoumia, lakini ukweli ni kwamba tunaumia kwasababu ya dhambi zetu, tunapaswa kukiri hili. Na kwakweli, kama tunashindwa kukubali dhambi zetu na madhaifu yetu, hatuna tofauti na viongozi hawa wa dini ya Kiyahudi. Tutakuwa tumebaki katika majivuno yetu na kujihesabia haki wenyewe.

Sala:
Bwana, jaza moyo wangu kwa unyenyekevu. Na kwa unyenyekevu, naomba unisaidie niweze kujiona mwenyewe kama nilivyo. Nisaidie niweze kuona dhambi yangu lakini pia unisaidie kuona juhudi zangu za kukutafuta. Nisaidie niweze kuacha dhambi zangu nikurudie ili niweze kufurahia furaha na uhuru wa kuingia katika Ufalme wako. Yesu, nakuamini wewe.
Amina.

Maoni


Ingia utoe maoni