Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumanne, Disemba 07, 2021

Jumanne, Desemba 7, 2021
Juma la 2 la Majilio

Isa 40: 1-11;
Zab 95: 1-3, 10-13;
Mt 18: 12-14


MUNGU ANATAFUTA KONDOO ALIYEPOTEA!
Karibuni sana wapendwa wa Bwana kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana katika somo la Injili, Bwana Yesu anatuhimiza tumkimbilie yeye, sisi sote tunaolemewa na kusumbuliwa na mizigo na matatizo mbalimbali kwani yeye ndiye mwenye kutupumzisha. Anatualika twende kwake, tukajivike nira yake, tukabebe mzigo ulio wake. Wengi wetu tunabeba mizigo mizito kweli ambayo siyo mali yetu na kwa hakika haitusaidii.
Tunajifunga nira za ulevi, mahusiano yasiyo rafiki, tunajifunga nira na marafiki wasiokuwa waminifu-wote hawa wametufanya tusumbuke na kulemewa na mizigo isiyo na faida. Wengi wetu tunachoka kwa sababu ya kubeba mizigo isiyo yetu. Upo msemo wa lugha ya kichaga usemao “Mshyahara wo isembo, ni ichoka.” Yaani, malipo ya mpumbavu ni kuchoka bila sababu. Mpumbavu hujiingiza kwenye matukio, na visa visivyomhusu. Hivyo mwisho wa siku hupoteza muda na rasilimali bila faida.
Yesu ndiye mwenye kutupatia ufahamu wa kutufanya tutambue yaliyo ya muhimu na kuyakumbatia. Tuache kukumbatia yasiyo ya muhimu. Tuondoe mizigo isiyo kuwa yetu.
Somo la kwanza Nabii Isaya anawaeleza wana wa Yuda walioko uhamishoni kwamba Bwana ndiye mwenye ukuu na mwenye kuwatuliza wote na kuwapatia faraja. Hakuna mwingine mwenye uwezo wa kufanya kama afanyavyo Bwana. Wana wa Yuda walimfikiria mungu wa Wababuloni kama Mungu mwenye uwezo na mamlaka ya kutuliza na kufariji kuliko Bwana Mungu wa Israeli. Lakini leo wanaelezwa kwamba hakuna aliye kama Bwana.
Ulimwenguni wapo wanaojidai kuwa na moyo wa kutaka kutuliza shida na matatizo yetu. Lakini tuwe makini na hawa kwani waweza kuwa na malengo yao binafsi. Wengi waliobembelezwa na wanadamu wameishia kutendewa unyama mkubwa. Sisi tumwamini Mwenyezi Mungu. Yeye ndiye mwenye kutubembeleza na kutufariji. Hakuna mwanadamu au kiumbe chochote chenye uwezo wa kumzidi Bwana. Hivyo tusichanganywe au kupoteza amani kutokana na maneno matupu ya mwanadamu mwenye kutaka kutubembeleza. Bwana Yupo na anapaswa awe wa kwanza.

Maoni


Ingia utoe maoni