Alhamisi, Novemba 25, 2021
Alhamisi, Novemba 25, 2021.
Juma la 34 la Mwaka
Danieli 6:12-28
Zab. 100 (K) Ufu. 19:9
Lk. 21:20-28
Hizi zitatufanya tuikose imani kwa hakika.
Karibuni sana wapendwa wa Bwana kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana leo katika somo la kwanza tunapata habari juu ya imani ya Daniel. Aliweza kuwa na imani kati kati ya wageni, wageni waliokuwa na roho mbaya juu yake, waliotaka aikane imani yake. Hivyo walimzunguka kila upande kwa sababu ya imani yake.
Leo tunasikia wakimshtaki kwa mfalme ili uhai wake uondolewe. Lakini Mwenyezi Mungu anakuwa upande wake. Daniel anamlimlia Mungu na kwa hakika anapata kuokolewa. Matendo ya kufanyiwa fitina kama alivyofanyiwa Danieli wanafanyiwa wengi kwa nyakati zetu.
Wapo kati yetu wenye umbea, wenye kufuatilia mambo ya watu, tusiotaka watu waishi bila uhuru, wafuatiliwe kila wanapokanyaga-kila wanachotenda kinaripotiwa-hakika hizi sio tabia za kimungu. Wanadamu wanapaswa kuishi katika uhuru, hata kama ni mke au mume anapaswa apewe uhuru na si kuishi kitumwa akifuatiliwa kama mhalifu. Hivyo tuwe watu wa kuwapenda wenzetu waishi kiuhuru, tusiwabane sana watu, tusiwe watu wa kutazama au kufuatilia kila kitu chao. Tabia za namna hii zinatufanya tutende dhambi kila siku.
Binadamu ni tofauti na simu yako au miguu yako ambayo kila wakati unapaswa kuitazama. Wanadamu wameumbwa ili waishi kwa uhuru. Tukiwa na tabia za kufuatilia kila ya mwenzetu hakika tutaishia kuwafitini na kuwaumiza wenzetu kila siku.
Katika somo la injili, Yesu anaelezea juu ya ujio wa nyakati ngumu kwa mji wa Yerusalem. Yerusalemu uliaminiwa kuwa mji wa amani lakini habari zinazoelezwa juu yake leo kwa hakika ni tofauti, sio habari za amani. Yerusalemu ilishindwa kupalilia amani yake kwa njia ya sala na kufanya toba na matendo mema. Mwishowe amani yao inachezewa na wao kuishi katika huzuni. Nasi tujitahidi kutambua kwamba tunaweza kuichezea amani yetu na kuishia kwenye magumu kama yaliyotokea kwa Yerusalemu, mji uliotangazwa kuwa mji wa amani.
Hivyo tusiwe watu wa kuendeleza siasa za chuki, za ukabila, unyanyasaji. Hizi zitatufanya tuikose imani kwa hakika. Tujitahidi kukuza amani. Tumsifu Yesu Kristo.
Maoni
Ingia utoe maoni