Jumanne, Novemba 23, 2021
Jumanne, Novemba 23, 2021
Juma la 34 la Mwaka wa Kanisa
Dan 2: 31-45;
Dan 3: 57-61 (K) 59;
Lk 21: 5-11.
KUJIANDAA KWA MWISHO WA ULIMWENGU
Karibuni sana wapendwa wa Bwana kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Katika somo la kwanza leo, Danieli anamfafanulia mfalme Nebuchadneza ndoto ya ajabu aliyoiona. Ndoto hii aliona sanamu kubwa, nzuri, iliyosifika sana. Ilikuwa imeundwa kwa fito za thamani na kwa hakika iliweza kutambulika na wengi. Lakini cha ajabu sanamu hii ilivunjwa vipande vipande kwa jiwe la ajabu lisilo kazi ya mikono ya mwanadamu lilipiga sanamu hii na kuivunja vipande vipande. Nafasi ya sanamu hii ilipotea.
Mwangavu wake na umaarufu wake na sifa zake zilipotea. Sanamu hii ni maono na ishara zenye kuashiria ujio wa nyakati za mwisho. Ni kiashirio cha falme na tawala zitakazoitawala dunia. Mwishowe tawala hizi zitaondoshwa zote. Atakayetawala ni Mungu mwenyewe. Ndio utawala utakaobakia milele. Ndio utawala wenye kuvunja vunja tawala nyingine za dunia.
Sisi tujifunze kumtumikia mwenyezi Mungu tuwapo hapa dunia. Tunaofanya kazi katika serikali na taasisi mbalimbali tujitahidi ili taasisi hizo ziishi kwa ajili ya Bwana na zimtumikie Bwana. Zisiendeleze uovu kwani tawala zote zilizo ovu zitashindwa mwishowe.
Tujitahidi kufanya mema. Tusiungane na wakorofi ili kukandamiza walio wadogo. Kila tulichonacho kimtumikie Bwana na kimfanye Bwana atawale.
Yesu katika injili anazidi kuelezea tena kuhusu nyakati za mwisho. Anazungumza kwa kulitolea mfano hekalu kwamba japokuwa lapendeza na kuwa na vitu vya thamani, kwa hakika itakuja siku moja vitu vyote hivyo vitaharibiwa. Dhahabu na vyote vilivyomo vitaachwa.
Kwa hakika Yesu alitumia mfano huu kuonesha kwamba mambo yote yatakuwa na mwisho, hata yale mazuri tunayoyajenga. Hivyo tujifunze kuthamini yaliyo ya Mungu kuliko yote. Tuache tabia ya kujitumikia sisi wenyewe tu. Pia tuwe makini tusirubuniwe na matapeli mbalimbali. Tujifunze kumtumikia Mwenyezi Mungu siku zote.
Tujiepushe kuwa watu wa tamaa na hivyo kufuata kirahisi maelezo ya matapeli. Tamaa zetu za kupenda mambo marahisi rahisi hutufanya tukamatwe kirahisi na matapeli. Tambua kila kitu ulichonancho kiwe kizuri namna gani, nyakati zitafika kila kitu kitabomolewa na kuondoshwa kitakacho baki cha maana ni imani yako kwa Bwana. Ilinde usiipoteze.
Maoni
Ingia utoe maoni