Alhamisi, Novemba 11, 2021
Alhamisi, Novemba 11, 2021.
Juma la 32 la Mwaka
Hek 7: 22 – 8: 1;
Zab 119: 89-91, 130, 135, 175 (K) 89;
Lk 17: 20-25.
UFALME WA MUNGU KATI YETU!
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo neno la Bwana tunaanza kwa kuliangalia somo la kwanza. Hapa tunakutana na fundisho juu ya hekima na hekima hii inavyoelezewa na tabia zake ama kweli ni hekima ya ajabu. Tunaambiwa kwamba ina nguvu ajabu, yaenea pande zote za dunia, yaweza kufanya upya vitu vyote, ndiyo inayowafanya watu wawe marafiki wa Mungu, inanguvu na yapita roho zote. Hii ndiyo hiyo hekima ndugu zangu.
Katika wimbo wa katikati, hekima hii inafananishwa na neno la Mungu. Hili ndilo lenye nguvu ya kutenda kama hii hekima hii tuliyoisikia katika somo la kwanza. Ndugu zangu hekima hii ni kitu gani? Ni Roho wa Mungu ndugu zangu. Unapo mchagua Mungu kuwa Baba yako, Roho yake huja na kukaa ndani yako, na kukuongoza namna ya kutenda. Ndio hii Roho ya Bwana ndugu zangu ifanyayo kazi ndani yako na hii ndiyo hekima yenyewe ndugu zangu. Na katika neno la Mungu hii hekima hupatikana kama tulivyosikia katika wimbo wa katikati kwani neno la Mungu lina Roho tena ni uzima. Neno la Mungu lenyewe limesheehini Roho ya Bwana, limebeba Roho yake ndugu zangu. Neno hili ni hekima kwani laweza kumwongoza mwanadamu katika maisha ya umilele.
Na hii ndiyo hekima inayopaswa ituongoze katika siku za mwisho wakati wa ujio wa utawala wa Mungu kama tunavyosikia katika injili ya leo. Hii ni kwa sababu utawala wa Mungu utakuja bila kutabirika na cha ajabu utawala huo Yesu anasema upo kati yetu tayari yaani yeye mwenyewe ndio huo utawala. Uwepo wake unatakiwa uchukuliwe kama sehemu yetu sisi ya kukesha kila wakati, kutokutumia muda wetu vibaya, kwani hakutakuwa na wa kutoa matangazo kama ya harusi au kipaimara ati yakitangaza ati ufalme wa Mungu umeshakuja. Kinachotakiwa ni kukesha na ile hekima ya Kimungu, kama tunayo ndiyo itakayotusaidia kuelewa hili. Kama hatuna hii hekima, nakwambia hatutaweza kabisa kufanya hili. Tutajikuta tunayumbishwa yumbishwa huko na huko kama makapi yapeperushwayo na upepo. Hekima hii ndiyo itakayotusaidia. Tusipokuwa na hekima tutakuwa tunayumbishwa na waalimu wa uongo.
Hivyo ndugu zangu tukazane kuomba hii hekima itusadie ili tupambane na dhoruba kama hizi tulizozisikia katika injili. Hekima hii tutaipata kwa kusoma neno la Mungu, kusali kila siku, kuungama na kutenda matendo mema. Ukifanya hivi, Roho wa Bwana anakuja na kukaa kati yako na kutenda pamoja nawe na kukuongoza mbele. Anakupatia nguvu ya kupambana na dhoruba mbalimbali za kimaisha. Unaepuka kuwa kama makapi. Ukiendekeza ulevi, masengenyo nakwambia hutaipata hekima hii.
Kingine ndugu yangu, ni kwamba injili ya leo inatuambia kwamba kwa kweli tujiandae kudanganywa. Wapo wengi watakaokuja wakitumia nafasi hii ya ujio wa Mungu ili kutishia watu, watu waogope, watetemeke na kumbe lengo lao ni kula pesa zao tu. Nakwambia ndugu yangu jiandae na watu kama hawa na wakija wapinge kisawa sawa.
Kingine ni kwamba kwa kweli kitendo cha kufanya suala la ufalme wa mbinguni liwe hivi limemfanya binadamu ajione kwamba kwa kweli yeye mwenyewe ni kiumbe dhaifu na hivyo yafaa azidi kuwa mpole kila wakati kwani hujui siku wala saa. Hivyo unapoishi duniani, ishi kipole, ishi vizuri na watu, usionyeshe aina yoyote ya ubabe. Tii hekima na sheria ya Mungu. Hii ni muhimu sana.
Maoni
Ingia utoe maoni