Jumanne, Novemba 09, 2021
Jumanne, Novemba 9, 2021
Juma la 32 la mwaka wa Kanisa
Sikukuu ya Kutabarukiwa kwa Basilika la Laterani
Ez 47:1-2, 8-9, 12;
Zab 45:2-3, 5-6, 8-9;
1Kor 3: 9-11, 16-17;
Yn 2:13-22
HEKALU LA MUNGU!
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo tunaadhimisha sikukuu ya kutabarukiwa kanisa la Laterano. Hili ni kanisa kuu la jimbo la Roma. Ndilo kanisa kongwe kwa upande wa wakristo wa magharibi; na lilijengwa na mfalme Constantino na mwanzoni kila aliyetaka kuwa mkristo ilibidi abatiziwe ndani ya hili kanisa na lilitabarukiwa na Papa Sylvester mwaka 324.
Hili huonekana kama kanisa mama na kuadhimisha sherehe yake kutabaruku ni ishara ya muungano wa makanisa yote chini ya kanisa moja na uongozi mmoja. Sherehe hii twasherekea ukuu wa Mungu wa kusimika jamii ya kiimani ndani ya ulimwengu huu, ni ishara wa uwepo wa jamaa ya Kikristo inayomwabudu Mungu wakati wote popote duniani. Sisi ni sehemu ya jamaa hii na hivyo lazima tuwe jamii yenye uhai, tusilegelege.
Siku ya leo masomo yetu ya leo yanatuongoza kutafakari sikuu ya leo. Zaburi ya leo ya wimbo wa katikati inazungumzia juu ya uwepo wa mto unaoupatia furaha mji ambapo Mungu ameweka makao yake. Huu mto ni neema za Mungu ambazo uwepo wake ni sababu ya mji huo kubarikiwa.
Mto huu katika somo la kwanza unaonyeshwa ukitoka katika hekalu la Mungu na kila maji yake yanapopitia panapata uhai na kuneemeka. Yote haya ni kutokana na nguvu za Mungu. Unabii huu wa Ezekieli katika somo la kwanza uliwahusu wana wa Yuda ambao kwa kipindi kirefu walitenda dhambi wakafukuza utukufu wa Mungu ndani ya lile hekulu.
Ukisoma sura ya 11 ya kitabu cha Ezekiel tunaanza kuona jinsi alivyoanza kuondoka hekaluni. Kitendo cha Mungu kutoka hekaluni, lile hekalu lilikosa nguvu na mji wote ukakosa nguvu na kusababisha kuangamizwa na Wababuloni. Kulitokea laana na shida.
Leo basi Mungu anarudi hekaluni na hakika kunakuwa tena neema. Na anadhihirisha kwamba kwa yeyote anayeshirikiana naye, popote pale walipo watabarikwa zaidi.
Hekalu letu ni kanisa letu ndugu zangu. Ndicho chanzo cha neema. Neema hizi tunazipata tukiwa katika muunganiko na kanisa, chini ya kiongozi mmoja Yesu Kristo anayewakilishwa na Papa kwa hapa duniani. Tuwe katika muunganiko na Kanisa tuzipate neema hizi, tukiwa mbali na kanisa ni chanzo cha sisi kukosa ulinzi na kubomoka kama ule mji wa Yerusalemu ulivyobomolewa na wababuloni kwa sababu Mungu alikosekana ndani yake. Walikosa ulinzi wa Mungu.
Yesu katika injili anadhihirisha kwamba hekalu lake ni nyumba ya sala na neema. Iheshimiwe na kutunzwa. Nasi tuyatunze makanisa yetu. Tusifanyie hapo biashara au harambee kiasi cha kuonekana kuwa nyumba ya biashara. Iwe sehemu ya kupatia neema.
Ukipewa nafasi ya kudeki kanisa usipige kelele tena kupiga michapo ndani ya kanisa, hata wakati mwingine kumsengenyea mtu ndani ya kanisa. Kanisa ni sehemu takatifu, usipatumie kutegesha mitego yako, kutafutia hapo mwanaume mzuri, au mwanamke mzuri, au unatembea bila heshima nk. Sehemu takatifu ni sehemu bora kuliko sehemu yeyote duniani.
Maoni
Ingia utoe maoni