Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Alhamisi, Novemba 04, 2021

Alhamisi, Novemba 4, 2021,
Juma la 31 la mwaka wa Kanisa

Warumi 14:7-12
Zaburi 27:1,4,13-14 (K)13
Luka 15:1-10

Ndugu zangu wapendwa, karibuni kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana leo, Mtume Paulo anawaeleza Warumi kwamba wao wanajulikana machoni pa Bwana. Maisha yao yote yapo katika mkono wa Bwana. Hata kama watakufa au kama wataishi, hakika bado wanazidi kubakia wa thamani machoni pa Bwana. Na kwa hakika hakuna hata unywele wa vichwa vyao utakaopotea au kusahaulika pale wawapo na Bwana.

Kristo anamiliki wote, waliokufa na wanaoishi. Hivyo hakuna haja ya kudharauliana au kuwahukumu wenzetu na kuwaona kama wasiofaa-wote ni wakristo. Hata kama ni wagonjwa kiasi kwamba hawawezi chochote, hata kama wana njaa ya ajabu, hata kama wanashindwa kupata mlo wa mchana, hata kama ni wadhambi kiasi gani-wote ni mali ya Mungu. Ni Mungu aliyewaumba ni mali yake.

Paulo anatoa ujumbe huu kwa Wakristo wa Roma kwa sababu kipindi walioongokea ukristo walikuwa watu wa aina mbalimbali. Baadhi walikuwa watumwa, wengine wagonjwa, wengine maskini-hivyo kulikuwa na urahisi wa kuanza kudharauliana na kuhukumiana. Pia kulikuwa na kishawishi cha wao kushindwa kukaa pamoja ndani ya kanisa. Yeye anawaeleza kwamba jueni kwamba wote ni mali ya Kristo. Hata kama nyumbani mwake hawezi kula nyama, anakula tu matembele bado anazidi kubakia mali ya Kristo.

Sisi tujifunze kuwapenda wote, tujue kwamba wenzetu hata kama wapoje wanazidi kubakia mali ya Kristo. Na hakika nao pia watauona wema wa Mungu kwani ni wana wake. Tujifunze kuwaheshimu wenzetu wote. Tuone aibu pale matabaka yanapoanza kuingia ndani ya kanisa, na watu kukoseana upendo na kuchukiana. Wenzetu wote ni mali ya Kristo. Tuwapende.

Katika injili, Bwana Yesu anazidi kutuonesha jinsi kila mwanadamu alivyo wa thamani machoni pa Mungu. Mungu yupo tayari kutumia gharama kubwa ili kumfanya asipotee. Tayari alikwishatumia gharama kubwa kwa kumtoa mwanae wa pekee ili amkomboe mwanadamu mtumwa.

Hivyo nasi tufuate mfano wa Mungu tuwaone wenzetu kuwa bado wanazidi kubakia wa thamani kubwa machoni pa Mungu. Tuwe watu wa kujitoa zaidi kwa ajili ya maendeleo ya wenzetu. Wenzetu wengi wanaumia kwa sababu bado hatujajitolea zaidi kwa ajili yao. Sisi tunatabia ya kujenga matabaka. Tunawapendelea watu wenye vyeo na sura fulani fulani. Wapo tunaopendelea wanadamu weupe, warefu na kuwachukia weusi na wafupi. Wapo tunaowastahi wenye fedha na kuwadharau walio maskini. Hatupaswi kuonesha hili. Tuwaheshimu wote. Tumsifu Yesu Kristo.

Maoni


Ingia utoe maoni