Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumamosi, Oktoba 23, 2021

Jumamosi, Oktoba 23, 2021
Juma la 29 la Mwaka

Warumi 8:1-11
Zaburi 24:1-2.3-4ab.5-6 (R. see 6)
Luka 13:1-9


TUMEITWA TUWE WAKAMILIFU!

Ndugu zangu wapendwa karibuni kwa adhimisho la Ekaristi Takatifu asubuhi ya leo. Katika somo la kwanza tunaona Paulo akiendelea kuwaasa Warumi kuhusu madhara ya kufuata vionjo vya mwili, mwili daima hupeleka mtu kwenye mauti kama utaufuata kwa kila kitu unachohitaji. Wakati roho inakuambia bia moja inatosha mwili unasema ongeza nyingine, mwili unataka ule tuu chakula na unatamani hata vitu vyenye sukari nyingi bila hata kujali kwamba ni madhara kwake wenyewe lakini ukitii hakika mwisho lazima mauti yaje haraka. Mwili unakusukuma nenda nje ya ndoa yako, haukutakii mema utapatwa na magonjwa na mwisho ni mauti.

Leo Paulo anatuasa nasi tusitumikie mwili bali tufuate sheria ya Kristo inayoongozwa na roho katika dhamiri safi. Kwa namna hiyo tutapata uzima na hatutakumbwa na mauti ya milele.

Ndugu zangu tujifunze kuwa na kiasi katika kuuthibiti mwili, kuuongoza na sio kuutii daima, kula kwa kiasi, kunywa kwa kiasi. Usile kila kitu, kuwa na muda wa kula pia usile hofyo hofyo nakunenepa nakupatwa na magonjwa. Tusiwe watumwa wa pombe, tusishindane na kiwanda cha bia. Usiwe mtumwa wa sigara nakupeleka mwili wako kwenye mauti.

Katika somo la injili Yesu anatoa mfano wa walioangukiwa na mnara na kufa kifo kibaya na kufundisha kwamba haimaanishi hawa wanaopatwa na mkasa huu ndio wadhambi.

Wakati mwingine sisi tunaobaki ndio wadhambi zaidi. Kile kipindi cha sisi tunabakia bila kuadhibiwa na tunabakia kusikia na kuona maumivu ya wengine ni kipindi cha kutufunza ili tuache dhambi. Ajali za wengine na mateso yao unayaona kwenye tv, au wakimbizi wakilia yote haya ni nafasi zitutakazo tuongeze bidii tuweka samadi ya kiroho. Ni kipindi ambacho tunatiliwa samadi kama huyu mkulima anavyofanya kwa huu mti wake ili tubadilike na tusipobadilika tutakatwa.

Wadhambi wengi tunaendelea kuishi kwa sababu ya huruma ya Mungu. Kati yetu tunaishi na watu ambao labda tungaliomba wawe wamekwishaadhibiwa tayari lakini Yesu anaruhusu waendelee kuishi ili basi wabadilike, ni huruma ya mkulima. Sisi tubadilike na tukiona hatujaadhibiwa tusijione ati sisi ni wajanja sana au Mungu hana nguvu. Mungu akiamua, nakueleza sisi hatutasalia. Tuombe kutumia nafasi tupewazo vyema. Wengi tunatumia vibaya kile kipindi Mungu anapokaa kimya na kuamua kumtukana na kumwona kana kwamba hana nguvu. Kwa hapa tunajilaani zaidi. Mungu ni mkuu kila wakati. Tuache kumkosea adabu.

Maoni


Ingia utoe maoni