Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumapili, Oktoba 24, 2021

Hamu ya kuuona Wokovu wetu–Yesu

Somo la kwanza kutoka Kitabu cha Nabii Yeremia, linaonesha upendo wa Mungu kwa wanadamu. Mungu anajulisha mipango yake ya kumkomboa mwanadamu. Anapanga kuwakusanya wote pamoja, kutoka pande zote za dunia, kama wagonjwa, vipofu, viwete, yatima na wajane; hataki kumwacha yeyote kwa sababu ya upendo wake wa kuokoa. Na hii ndio sababu ya furaha, kuimba na kushangilia, kwa sababu Mungu anatuchukua sisi kama watoto wake na anatupa upendeleo wa kumuita yeye Baba yetu. Ahadi hii ilikuwa ni tumaini kubwa kwa wana wa Israeli kwani baada ya utumwa wa Babeli walitapakaa katika nchi mbali mbali. Mungu anatoa matumaini ya kuwakusanya tena kama wanae.

Katika somo la Injili leo, tunaona Imani ya kipofu Batimayo aliyekuwa akisubiri wakati wa wokovu. Alikaa pembezoni mwa barabara akiomba. Watu wengi walikuwa wakitembea wakisafiri pamoja na Yesu na walimkaribia Batimayo. Yesu inawezekana alimuona Batimayo au kwa sababu ya watu wengi, hakuweza kumuona. Batimayo anawasikia na anaanza kujongea kumfuata Yesu. Ana mtambulisha Yesu kama “Mwana wa Daudi” [jina la Masiha ambaye angekuja] akimtambua Yesu kuwa Masiha-Kristo. Umati wa watu walimzuia wakimnyamazisha Batimayo, lakini yeye alipaaza sauti zaidi akiomba msaada. Lakini Yesu alikisikia kilio chake cha uchungu, na anasema “Mwiteni.” Wanamleta kwa Yesu. Kinachofuata ni kuponywa. Yesu anamwambia “Nenda Imani yako imekuponya.” Na mara anaweza kuona tena na Batimayo anafuatana nao wakitembea barabarani.
Katika mtazamo wetu wa sasa, sisi pia tupo kama yule kipofu. Upo umati, hisia, marafiki, kazi n.k, vinavyo tufunga tushindwe kumfikia Yesu vizuri. Tunamsikia Yesu akipita karibu nasi, kwa Injili tunayoisikia Kanisani, katika nyimbo mbali mbali za dini, nyingine tunazo pokea kupitia Facebook, WhatsApp, n.k, je tunawashirikisha na wengine au tunawazuia kama ule umati? Tujaribu kufikiria ni mara ngapi Yesu ametupita kwa sababu hatumuiti na kumlilia kwa mahitaji yetu. Je, unataka kubakia bila kupata upendo wa Yesu? Yesu anatusubiri tumuite.

Marko, katika Injili, anaonesha kwamba tendo hili lilitokea wakati Yesu na umati wa watu walipokuwa wanauacha mji (Mk 10:46). Ni mawazo mazuri ingawaje Yesu alikua njiani kuelekea Yerusalemu kuteswa, alipata muda wa kusimama na kumuita Batimayo, na kumuuliza alitaka nini kutoka kwake. Chochote alicho fundisha wakati akitembea, vilisahaulika kwa kwa sababu ya mahitaji ya watu. Usije ukafikiria hata siku moja ya kwamba Yesu hana muda na hitaji lako. Koti lilitupwa pembeni. Hakuwa na jambo lingine la kuhangaikia koti lake. Koti, pengine linawakilisha maisha yake ya zamani, na sasa Yesu ndiye maisha yake mapya.

Kwa sababu alikuwa kipofu, watu walimuongoza kwenda kwa Yesu. Lilikuwa jambo nzuri kuhusu hitaji lake, kwa nini Yesu alimuuliza alitaka nini kwake? Maisha yake yalikuwa tegemezi sana kwa wengine kwa hiyo yalibadilika kwa sababu aliponywa. Watu bado wangefikiria kipindi chake akiwa anaomba kabla ya kuponywa. Hangehitaji tena kuomba, je ni jambo hilo alilolitaka kweli? Mara nyingi Yesu anatutaka tuweke katika maneno dhahiri tunalohitaji kwake. Anatazama aweze kuona ni kwa jinsi gani mioyo yetu inaendana na kile tunachotaka afanye kwetu. Ninaogopa ninachokiomba hakijibiwi kwa sababu sina uvumilivu. Moyo wangu lazima uwe na kile nikiombacho. Vipi kuhusu hali yako binafsi? Ni mara ngapi unaingia ndani ya maisha yako ya sala? Moyo wa Batimayo ulikuwa ndani ya kile alichokiomba kwa Kristu. Ulijawa na nguvu na shauku. Uwezo wake wa kuita bila kukatizwa na sauti za watu au vitu ni muhimu sana katika maisha ya sala. Yesu anamkuta mtu huyu akiwa katika hitaji kubwa na asingeweza kumpita tu.

Batimayo hakuwahi kumuona Yesu, alichojifunza kuhusu Yesu ilikuwa tuu yale aliyo simuliwa na wengine. Wakati watu walipo mwambia “jipe moyo! Simama anakuita”
(Mk 10:49), aliamini ushuhuda wao, akatupa koti lake wakamuongoza kwenda kwa Kristo. Je, unaweza kumuona Yesu pia kwa jicho la Imani?

Alichofanya kwa Batimayo anaweza kufanya pia kwako. Yesu alipomaliza kusema maneno “upate kuona, Imani yako imekuponya” macho ya kipofu yalifunguka akaweza kumuona…Mkombozi wa Ulimwengu, Yesu, yupo tayari kufungua upofu wetu pia. Tupo tayari kupokea na kukaa katika upendo wake na utukufu wake? Tulisikie neno lake na kutupa koti la dhambi zetu na kumfuata.

Sala: Bwana, fungua macho ya moyo wangu, nataka kukuona,

Amina

Tumsifu Yesu Kristo...

©️Pd. Prosper Kessy OFMCap.

Maoni


Ingia utoe maoni