Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatano, Oktoba 06, 2021

Jumatano, Oktoba 6, 2021.
Juma la 27 la Mwaka

Yon 4: 1-11;
Zab 85: 3-6, 9-10;
Lk 11: 1-4


NAMNA YA KUSALI

Karibuni ndugu zangu katika adhimisho la Ekaristi asubuhi ya leo. Neno la Bwana tunaaza kwa kuliangalia somo la kwanza. Hapa tunamkuta Nabii Yona akihuzunika-kwa sababu ati Mungu amesikiliza toba ya watu wa Ninawi na hivyo kuwaondolea ile adhabu ambayo ingewapata. Wanasamehewa, hawaangamizwi tena. Yona anakasirika kwa nini Mungu anahuruma hivi? Kwa nini asingewaangamiza?

Mungu anaukataa ubinafsi wa huyu Yona. Anamwambia kwa nini yeye anaona kwamba mti unayodhamani kuliko mji wa ninawi-kwa sababu uchungu anaoupata kwa ule mti kukauka-ni mkubwa kuliko ambao angeupata kama watu wa ule mji wangeteketezwa. Mungu anamwambia kwamba-watu wa Ninawi wana nafasi kuliko ule mti.

Huku kujiepusha na ubinafsi ndiko tunakokukuta tena katika injili ya leo Yesu anapofundisha sala ya Baba yetu. Anatumia sala hii kuwafundisha kusali na utaona katika sala hii anakataa ubinafsi moja kwa moja. Mfano, inasema moja kwa moja kwamba usipomsamehe mwenzako, nawe pia husamehewi, kipimo unachopima kwa mwenzako, ndicho utakachopimiwa na wewe. Hiki ndicho Yona anachoambiwa tena na Mungu katika somo la kwanza.

Ndugu zangu, masomo haya yanasema mengi hasa kwetu sisi ndugu zangu. Kuna watu wasiotaka wengine nao mambo yawaendee vizuri. Kama wao walingatwa na nyuki au manyigu-atahakikisha anakudanganya danganya-anakupitisha njia ambazo nawe utangatwa na nyuki au manyigu na hiyo ndiyo furaha yao, hapo ndipo watakapofurahi na kucheka-watakupitisha njia ambayo kama wao walifukuzwa na mbwa mwenye kichaa-basi wanataka na wewe ufukuzwe naye-haya ndiyo maisha.

Nakwambia ndugu zangu tuache ubinafsi huu. Furahi ukiona mwenzako mambo yakienda basi vizuri-kama wewe ulipata mateso-yachukulie yawe fundisho kwamba sitaki mwenzangu naye ateseke kama nilivyoteseka. Fanya hivyo ndugu yangu. Usitake kuona ati na mwenzangu naye anateseka ndio ufurahi.

Kingine ni kwamba katika sala yako, hakikisha Mungu anatukuzwa-si kujitukuza wewe, halafu angalia kwamba mapenzi ya Mungu yanatimizwa na nia zako mbaya zinaachwa. Hii ndiyo namna ya kusali tunayofundishwa leo.

Usitegemee kusali ukiomba Mungu amvunje mwenzako miguu au Mungu ampofushe mtu fulani au amfanye awe kiwete utegemee Mungu atakusikia. Mungu husikia maombi mema na nia njema. Tumsifu Yesu Kristo.

Maoni


Ingia utoe maoni