Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumanne, Septemba 21, 2021

Jumanne , Septemba 21, 2021,
Juma la 24 la Mwaka

Sikukuu ya Mt. Mathayo, Mtume na Mwinjili

Efe 4:1-7, 11-13
Zab 19:1-4
Mt 9: 9-13

MUNGU HAWAITI WAKAMILIFU,
ANAWAPA UKAMILIFU WALE ALIO WAITA

Ndugu wapendwa, karibuni kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana katika asubuhi ya leo tunapoadhimisha sikukuu ya Mt. Mathayo tunakutana na ujumbe maalumu toka katika somo la kwanza, Paulo anawaeleza Waefeso kwamba wajitahidi kuwa waaminifu katika wito walioitiwa. Wanaelezwa wajione kama sehemu ya mwili wa Kristo, yaani kanisa. Hivyo kama kiungo, kila mmoja amekabidhiwa nafasi yake, kila mmoja anao umuhimu wao. Uzembe kidogo wa kiungo kimoja utakosesha mwili wote nguvu.

Hivyo siku zote wakristo wanapaswa kujiona kuwa wamoja, mwili mmoja wanaojenga kitu kimoja chenye faida kwa wote. Ujumbe huu unamhamasisha kila Mkristo awe mtu wa kujitahidi. Mt. Mathayo alitambua hili ndugu zangu, Mt. Mathayo baada ya kutambua hili, alijitahidi sana kuishi nafasi yake kama kiungo muhimu cha Kristo. Aliandika injili yake kwa kiebrania kwa lengo la kuwavuta Wayahudi kwenye imani.

Sisi tunapokumbuka Mt. Matayo, tuombe kutambua kwamba sisi ni sehemu ya mwili wa Kristo, yaani kanisa. Hivyo tufanye yote kwa heshima ya Kristo na kanisa lake. Tuondokane na kiburi au kufanya mambo yetu kibinafsi, ungana na kanisa katika shughuli zako. Kabla ya kufanya uamuzi wetu wote, lazima tujitafiti na kuona kwamba je, sisi kama wana wa kanisa, uamuzi huu utalisaidia vipi kanisa, au utaliharibu vipi kanisa? Sisi ni viungo wake. Wengi wetu wanafanya maamuzi mabovu baada ya kusahau kwamba wao ni wana wa kanisa. Kama wana wa kanisa, hatupaswi kutembea wenyewe, tunapaswa kutembea na kanisa.
Liruhusu kanisa liwe rafiki kwako.

Katika injili, Yesu anamwita Matayo kuwa mtume wake. Anamkuta katika ofisi ya mtoza ushuru na hapo anamwita katika kazi yake hiyo. Yesu anapofanya tukio hili anapata marafiki watoza ushuru wengi. Yesu anasema waziwazi kwamba hakuja kuwaita wenye haki bali wadhambi wapate kutubu.

Huyu Matayo mtoza ushuru anapoitwa, na kuguswa na Yesu kwa namna ya pekee, anakuwa tayari kuacha kazi yake, japo ya faida kwake kidunia na kumfuata Yesu. Hili tukio liwe somo kwetu. Wengi wetu tupo kama huyu Matayo kwani bado tuna tozo za ziada, tozo za zaidi tunazowafanyia wenzetu, ujira wa ziada, dhuluma tunaowafanyia wenzetu na Yesu anakuja kwetu kila siku kwa namna ya pekee akitutaka tuache tozo hiyo na kumfuata. Lakini wengi wetu tunafurahia hiyo tozo, tunafurahia hiyo dhambi na kuona kwamba kwa sababu tunaendelea kufaidi, kuishi maisha mazuri kutokana na hiyo dhuluma yetu au tozo ya ziada, hatupo tayari kuacha.

Maisha ya namna hii, yatatuangusha ndugu zangu. Tuwe hodari kama Matayo. Alikuwa tayari kuacha kile kilichokuwa kinampatia raha, kafaida cha kidunia. Nawe usione haya kukaacha. Hako ndicho kanachokuangusha. Kisikufanye wewe uchelewe kufanya maamuzi. Unapaswa kufanya maamuzi sasa. Acha hako katabia.

Maoni


Ingia utoe maoni