Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Alhamisi, Septemba 16, 2021

Alhamisi , Septemba 16 2021,
Juma la 24 la Mwaka wa Kanisa

Karibuni sana wapendwa wa Bwana kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana leo katika somo la kwanza, Paulo anamwagiza Timotheo juu ya tabia za anayepaswa kuwa mtumishi wa Bwana, askofu, lazima awe mtu mwenye tabia na maadili mema ili aweze kulitia moyo taifa la Mungu.

Ukweli ni kwamba bila maadili, taifa la Mungu hupotea. Wana wa Sodoma na Gomora waliangamia kwa sababu walikosa maadili mema. Askofu anapaswa kuwa mwalimu wa maadili, ili aiokoe jamii isiangukie katika mkondo wa kupotea na kuja kuadhibiwa kama watu wa Sodoma na Gomorah. Hivyo tutambue nafasi ya viongozi wetu wa kanisa, na tupokee ushauri wao pale wanapotukosoa. Lakini ugumu kanisa linalokumbana nao ni kiburi toka kwa baadhi ya kondoo wake.

Wapo kondoo wenye majivuno, wenye kujiona kuwa wajuaji na wasiojali. Wanajiona kujua maadili na mafundisho kuliko hata viongozi wa kanisa wenyewe. Wanapotufundisha juu ya kuacha uchumba sugu, juu ya kuacha uasherati, juu ya kulisaidia kanisa, wengi wetu tunadharau na mioyo yetu haijali. Tuepukane na tabia za namna hii. Tusifikiri kwamba kwa viongozi wetu wa kanisa kukaa kimya na kufumbia macho maovu yetu, ndiyo hali itakuwa na amani. Ukweli ni kwamba ukikaa ndani ya jamii ambayo hakuna anayetupinga au kutukosoa ni dalili ya uwepo wa shetani ndani ya hiyo jamii, mwenye kutufanya tujisikie kuwa salama na huru lakini kwa kiasi kikubwa bado tupo gizani.

Watu wa Sodoma na Gomora waliangamia kutokana na uzembe wa namna hii. Sisi tufurahie pale tukutanapo na watu wenye kutukosoa. Wapo wazazi, ndugu, viongozi na waalimu. Wanapotukosoa, tusikasirike au kuanzisha kisasi nao. Tuwapokee na hakika maisha yetu yataimarika.

Katika somo la injili, Bwana Yesu anamuonea huruma mjane wa Naini na kumpatia uhai mtoto wake aliyefariki. Yesu anamuonea huruma mama huyu, anahuzunishwa na machozi yake na ukiwa wake. Hakika Yesu huona machozi na ukiwa wetu. Tukimlilia kama alivyofanya yule mjane wa Naini hakika atatuonea huruma kama alivyoweza kumwonea huruma mama huyu. Hivyo tusiache kupeleka huzuni zetu na masikitiko yetu kwa Bwana Yesu. Hakika atatusikiliza kama alivyomwonea huruma na kumsikiliza mama huyu. Nasi tumwombe apate kutuonea huruma leo. Tumsifu Yesu Kristo.

Maoni


Ingia utoe maoni