Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Alhamisi, Septemba 02, 2021

Alhamisi, Septemba 2, 2021
Juma la 22 la Mwaka wa Kanisa
Sala ya Kanisa (Zaburi)-Juma la 2

Kol 1: 9-14;
Zab 98: 2-6;
Lk 5: 1-11


NGUVU YA NENO LA YESU!
Karibuni sana wapendwa wa Bwana kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana katika somo la injili, tunakutana na Yesu akiingia katika mateso na shughuli za akina Simoni. Anawakuta katika changamoto ya kupambana, wakivua samaki bila kupata kitu. Yesu anawapatia maelekezo ya kufuata na hakika kwa njia ya yale maelekezo, wanafaulu kwa kiasi kikubwa, kuliko hata walivyowahi kuona katika historia yao ya uvuvi.

Wao walizoea kuvua usiku kwani waliamini kwamba samaki hupatikana kwa wingi usiku kuliko mchana. Lakini Yesu anawaeleza wavue mchana na kwa neno lake wanavua samaki wengi kuliko walivyozoea kuvua usiku. Hakika neno la Bwana lina nguvu ajabu. Kwa neno lake twaweza kufanya maajabu mengi. Neno hili litutie moyo kuanza shughuli zetu kwa jina la Bwana. Tusianze chochote bila kulitaja jina la Bwana. Bila jina la Bwana, tutavua usiku kucha bila kupata chochote kama ilivyotokea kwa akina Petro.

Yesu katika injili, anawaeleza akina Petro kwamba atawapa kazi mpya, kazi ya kuvua watu, kuwa wavuvi wa watu na si samaki tena. Hii yamaanisha kwamba hakika Bwana Yesu aliwapatia kazi yenye hadhi, kazi ya kuvua wanadamu. Sisi ndugu zangu, tumwombe Bwana Yesu atupatie kazi yenye hadhi. Mara nyingi tunatumia muda wetu kwa mizaha, kusengenya wengine na kutoa porojo nyingi. Bwana Yesu atatuonesha kazi zenye hadhi-ambapo tutaweza kufungua macho na kuona mahitaji ya wenzetu, na kuwasaidia. Sisi tuombe ili tuweze kufaidika kwa kazi za namna hii.

Katika somo la kwanza, Paulo anawaombea wakristo wa Kolosai na kuwatakia matashi mema. Anasali kwa ajili yao, wapate kumtambua Mwenyezi Mungu, watimize wajibu wao kwa Bwana na kuzaa matunda mema kwa ajili ya kazi njema. Naomba sala na maneno haya ya Paulo yatubariki na sisi. Tunahitaji kuombewa na kutakiwa matashi mema kama Paulo anavyofanya. Nasi tuwe watu wa kuongea ujumbe wa matumaini kwa wenzetu kama alivyofanya Paulo. Tuepuke kuwatukana wenzetu au kuwasema vibaya bali tuwapelekee ujumbe wa matumaini kama anavyofanya Paulo leo.

Maoni


Ingia utoe maoni