Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatano, Agosti 18, 2021

Jumatano, Agosti 18, 2021
Juma la 20 la Mwaka
_______

Amu 9: 6-15;
Zab 20: 2-7;
Mt 20:1-16
_______

JE, UNAKUWA NA WIVU MWENZAKO ANAPO FANIKIWA?

Karibuni sana ndugu zangu wapendwa kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Leo neno la Bwana katika somo la kwanza tunakutana na wana wa Israeli wakiwa katika nchi ya ahadi; hakika wanashindwa kuifurahia nchi hii. Kile walichoahidiwa hawakioni kwa sababu wameyakiuka maongozi ya Mungu. Wanaishi kwa kuyaiga mataifa mengine yaliyowazunguka. Wao walifikiria kwamba mataifa mengine yalifurahia kwa sababu wao walikuwa na mfalme.
Kitendo cha wao kukosa mfalme wa kibinadamu kama hayo mataifa mengine kiliwafanya wajifikirie kwamba ndio sababu za wao kushindwa kuishi maisha ya raha. Na leo wanajichagulia mfalme aliyeitwa Abimeleki. Na huyu mfalme kwa hakika alileta shida badala ya raha kwa wana wa Israeli. Huyu mfalme atawaletea moto badala ya kuwapa utulivu.
Ndugu zangu, haya ndio matokeo ya kuzitegemea nguvu zetu na kuacha kumtegemea Mwenyezi Mungu. Kile tunachokichagua, tunachokiona kuwa chema kumbe tunakikuta kuwa hatari kubwa, yenye kuiletea maisha yetu maangamizi kama Abimeleki alivyokuwa kwa wana wa Israeli. Hivyo tuache kuzitegemea nguvu zetu zaidi kuliko kumtanguliza Mwenyezi Mungu mbele.
Wengi wetu tumeanguka kwa sababu ya kujiamini kupita kiasi. Tukumbuke udhaifu wetu na kuwa wapole na wenye hekima zaidi.
Katika somo la injili, Yesu anatoa mfano wa wafanyakazi waliokwenda katika shamba la mizabibu na kulipwa mshahara mmoja. Yawezekana wale waliofika mara ya mwisho walionesha nia ya kufanya kazi kwa bidii zaidi na ndani ya muda mfupi, nia yao iliweza kumfurahisha mwajiri kuliko walivyokuwa wale wa kwanza. Wale wa mwisho hakika walikuwa na nia ya kufanya kazi kwani walikuwa tayari kukaa sehemu ya soko hadi jioni wakiwa wakitafuta kazi. Hivyo mwajiri alifurahishwa sana na nia na utayari wa hawa waliokuwa tayari kufanya kazi.
Hakika Mwenyezi Mungu naye huangalia nia na utayari. Utayari wa namna hii na bidii ndio utakaotufanya tuingie mbinguni. Hivyo tuwe na nia na bidii na utayari wa kufanya kazi katika shamba la Bwana. Shamba la Bwana lina wafanyakazi wengi lakini wengi wetu hatuna nia ya kufanya kazi. Tuwe na nia ya kufanya kazi kama wale wafanyakazi ambao walikuwa tayari hadi mwisho. Tumsifu Yesu Kristo.

Maoni


Ingia utoe maoni