Jumanne, Agosti 17, 2021
Jumanne, Agosti 17, 2021
Juma la 20 la Mwaka
Amu 6: 11-24
Zab. 85: 8, 10-13
Mt. 19: 23-30
Ni yule anayejali mali kuliko Mungu.
Karibuni sana ndugu zangu wapendwa kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana leo katika somo la kwanza Mwenyezi Mungu anawakumbuka wana wa Israeli wakiwa katika nchi yao ya ahadi. Huku katika nchi ya ahadi, hawafurahii kama walivyofikiria pale mwanzo kwamba itakuwa sehemu ya kula na kunywa maziwa na asali. Wanajikuta tena wakiwa tena watumwa ndani ya nchi yao wenyewe waliopewa na Bwana. Yote haya ni kwa sababu ya kiburi chao ndugu zangu.
Wao wamemwacha Bwana Mungu wa Israeli na kwenda kuitumikia miungu mingine. Ndipo walipojikuta wakiingia katika utumwa. Ndugu zangu, wana wa Israeli walikombolewa sio tu kimwili bali kiroho pia. Mwenyezi Mungu alipowatembelea kule Misri, hakuwakomboa kimwili tu, bali aliwapatia pia ukombozi wa kiroho, Mwenyezi Mungu alipata kujitambulisha kwao kuwa ndiye Mungu wao, na hivyo akawaokoa katika utawala wa Ibilisi. Kosa la wana wa Israeli ni kwamba wao walikuwa wakijirudisha katika utumwa kwa kuanza kuiabudu tena miungu ya kipagani na sanamu. Utumwa huu uliwafanya pia watekwe kimwili. Hivyo walipaswa kujitoa katika utumwa wa kiroho, wazipatie roho zao uhuru na ndipo pia waipatie miili yao ukombozi pia.
Sisi ndugu zangu tutambue kwamba tutakuwa na ukombozi kweli pale tutakapothamini ukombozi wetu wa kiroho.Tutakapozikabidhi nafsi zetu kwa shetani tena ndipo tutakapokuwa watumwa kwa kila kitu. Jamii yetu, familia itakuwa watumwa. Tutajisikia watumwa wa kila kitu. Hivyo kila mmoja wetu tujitahidi kudumisha na kuupenda uhuru wetu wa kiroho. Huu ndio ukombozi wa kweli.
Katika somo la injili, Yesu anaelezea juu ya ugumu uliopo kwa tajiri kuingia katika ufalme wa mbinguni. Anaeleza hili kwa kusema kwamba ni rahisi hata kwa ngamia kupenya katika tundu la sindano kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa mbinguni, tujiulize, tajiri ni mtu gani? Ni yule anayejali mali kuliko Mungu. Hivyo ataona afadhali atumie muda wake kwa biashara zaidi kuliko kwa ajili ya Mungu. Machoni pake faida ni kubwa kuliko utu wa mwanadamu mwenzake. Anaona thamani katika mali yake kuliko katika mwanadamu mwenzake, yuko tayari kumwona mwenzake anakufa njaa kuliko kumpatia kidogo ambacho kingalimpatia uhai. Huyu ndiye tajiri; mwenye kuona thamani katika mali kuliko katika wanadamu wenzake au katika Bwana.
Watu wa namna hii sio lazima wawe na mali nyingi; wapo ombaomba wenye roho za namna hii. Hawa pia itawawia vigumu kwao kuingia katika utawala wa mbinguni. Tunapaswa kuwa na roho ya ukarimu, yenye kumjali Mwenyezi Mungu na jirani zetu pia. Hapa tutaweza kuzikomboa roho zetu na utumwa wa mali.
Maoni
Ingia utoe maoni