Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumamosi, Agosti 14, 2021

Jumamosi, Agosti 14 2021
Juma la 19 la Mwaka

Kumbukumbu ya Bikira Maria
___________

Yos 24: 14-29;
Zab 15: 1-2, 5, 7-8, 11;
Mt 19:13-15
_______

KUMPOKEA YESU KAMA WATOTO!
Ndugu zangu wapendwa, karibuni kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana, katika somo la kwanza, Yoshua anawaeleza wana wa Israeli kwamba yeye na familia yake watamtumikia Bwana. Kwa nini Yoshua aseme yote haya? ni kwa sababu kipindi hiki wapo katika nchi ya ahadi, na hapa wanafurahia maisha, hawapo tena katika jangwa.
Kilichotokea ni kwamba kuna kizazi kilichozaliwa katika nchi ya ahadi ambacho hakikuyaona maajabu ya Mungu tangu walipokuwa Misri. Wala hakikujua kwamba baba zao walipata shida jangwani na kusaidiwa kwa nguvu ya mkono wa Mungu. Wao walianza kuambatana na baadhi ya makabila ambayo hata hapo mwanzoni yalikuwa maadui yao, makabila ambayo yalikuwa hayataki wana wa Israeli waingie hata katika nchi ya ahadi. Walianza kukumbatia tamaduni zao, na kuoa na kukubali kuolewa nao. Joshua anatoa onyo kwa watu wa namna hii.
Anawaeleza kwamba ulizeni historia yenu, ulizeni jinsi mlivyowahi kusaidiwa na Bwana. Hivyo msimwache Bwana Mungu wenu.
Ujumbe huu utusaidie na sisi pia. Tuwe watu wa kuulizia historia zetu. Wapo baadhi yetu ambao tumezaliwa na kukuta wazazi wetu wametuandalia mambo mazuri, lazima tuwe tayari kuuliza haya mambo mazuri yalianzaanzaje, tusianze kutumia tu bila kujikumbushia historia ya vitu unavyotumia. Wapo pia ambao wameolewa na kukuta mambo mazuri, lazima tuwe tayari kuuliza huyu mtu alianzaanzaje akafikia hapa? Usianze kutumia bila kuulizia historia. Historia itakufanya mnyenyekevu na kumkumbuka Bwana Mungu wetu; kwa sababu wengi wetu historia zetu ni dhaifu na zenye kutunyenyekesha.
Katika somo la injili, Yesu anasema kwamba ufalme wa mbinguni ni kwa ajili ya wale walio kama watoto. Watoto ni wanyenyekevu na wenye matumaini makubwa. Huwa wakifundishwa-wanaamini haraka. Sio wepesi wa kupinga ujumbe au fundisho hasa wakijua kwamba latoka kwa wazazi wao au watu wao wa karibu. Mungu ndiye mtu wetu wa karibu. Lazima tuwe tayari kupokea maagizo yake na mafundisho yake kama watoto wadogo. Hii ndiyo imani, hapa ndipo kujijengea baraka, hapa ndipo kuwa mkubwa katika ufalme wa mbinguni.

Maoni


Ingia utoe maoni