Jumamosi, Julai 24, 2021
Jumamosi, 24 Julai, 2021,
Juma la 16 la Mwaka
Kut 24:3-8;
Zab 34:1-10
Yn 11:19-27
Karibuni sana wapendwa wangu kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Leo tunaadhimisha kumbukumbu ya Wat. Yoakimu na Anna, Wazazi wa Mama Bikira Maria. Wazazi hawa wanaheshimika kwa sababu wamekuwa sababu ya mtoto wao, Maria, aliyekuja kuwa Mama wa Mkombozi wetu Yesu Kristo.
Wazazi hawa walijitahidi kumtunza mpendwa wa Mungu, mnadhiri wa Mungu na hakika akafanikiwa kuja kuwa mama wa Mkombozi wetu Yesu Kristo. Ni somo na fundisho kwetu, kuwatunza wapendwa wa Bwana. Wale wanaoonesha nia ya kumtumikia Mungu, yafaa tuwatie moyo, tuwapatie mazingira bora, tuwaepushe na mazingira yaliyojaa maneno machafu. Tuepuke kuwakwaza wale wanaopenda kumtumikia Mwenyezi Mungu kama alivyofanya Mama Maria. Mapokea yanatueleza kwamba wazazi hawa walimpeleka mtoto wao, yaani Maria katika hekalu na huko alianza kujifunza maisha ya kumtumikia Mungu tangu utoto wake. Hii ilikuwa hazina kubwa kwake kwani ilimfanikisha sana maishani na kuishi maisha ya amani.
Sisi kama wazazi tutambue kwamba miongoni mwa zawadi kuu tuwezazo kuwapatia watoto wetu na vijana wetu ni zawadi ya kumpenda Mungu. Ukiona kijana au binti yako anampenda Mungu, hapa ndio unaweza kusema kwamba umefaulu. Kwa sababu asiyejali, asiyemjua Mungu huwezi kumtegemea kwa lolote. Anaweza kuwa na uwezo kifedha lakini haaminiki au huwezi kumtegemea kwa lolote. Lakini kama anamfahamu Mungu, na anajali, hii ndio zawadi kubwa tuwezayo kumwachia. Na kwamba unamuacha mtu ambaye anaaminika, anaweza kutekeleza kazi, na kuwa mwanga kwa wenzao.
Sisi tujifunze kuwaachia watoto wetu urithi wa kumcha Mungu. Uwe urithi wetu.
Katika somo la injili, Yesu anawaeleza wanafunzi wake kwamba heri macho yao kwa kuwa yanaona na kusikia yale wanayoyasikia sasa. Wapo wengi waliotamani kukutana na Yesu na kumuona akifanya kazi ya umasiha. Yesu alizaliwa na Bikira Maria na Maria alikuwa mtoto wa Yoakimu na Anna. Hivyo Yesu alikuwa sababu ya Mama Maria, pamoja na Yoakimu na Anna kupata sifa kuu. Sisi tutambue kwamba maadili yetu mema na maisha yetu yenye adili yatawafanya wazazi wetu na ndugu zetu wapate sifa. Maisha yetu mabaya ni sababu ya wazazi wetu na pia ndugu zetu kupata sifa mbaya na kuishi katika huzuni. Tuishi kimaadili kadiri ya Injili tunayosikia sasa ili tuweze kuwa sababu ya furaha kwa vizazi vyetu.
Tumsifu Yesu Kristo
Maoni
Ingia utoe maoni