Jumatano, Julai 21, 2021
Jumatano, Julai 21, 2021.
JUMA LA 16 LA MWAKA
Kut 16:1-5, 9-15;
Zab 78:18-19, 23-28;
Mt 13:1-9.
MBEGU NENO LA MUNGU!
Karibuni sana ndugu zangu wapendwa kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Leo katika tafakari ya Neno la Bwana, wana wa Israeli wanapatwa na njaa jangwani na kuanza kutamani utumwa. Wana wa Israeli walipotoka Misri, walibeba vyakula mbalimbali lakini kwa wakati huu, vimeisha. Wanalalamika na kuanza kutamani chakula cha Wamisri.
Mungu atawanyeshea mkate safi, mkate toka Mbinguni, Mana ili waile. Lakini muda sio mrefu, watakinai chakula hiki na kuanza kutamani kile cha utumwani Misri na kusema ni kizuri zaidi. Na Mwenyezi Mungu atakasirika na kuwaadhibu na mwishowe wale wote watakaokataa kuila manna, watashindwa kufika katika nchi ya ahadi.
Ndugu zangu, sisi changamoto kubwa inayotukabili kila siku ni kukinai sakramenti. Mara ya kwanza, tunapokea sakramenti zetu kwa mwitikio mzuri, lakini baada ya muda, tunaanza kukikanai na mwishowe nafasi ya skaramenti zetu inapotea. Hili ni suala tunalopaswa kupambana nalo kwani wakristo wengi wameacha kupokea sakramenti, hasa ekaristi kwa sababu wanadai hawaoni chochote cha ziada. Wamekinai sakramenti hii. Lakini wanapaswa kuelewa kwamba sakramenti ni mafumbo matakatifu yanayopaswa kupokelewa kiimani. Bila imani, huwezi kuiona nguvu ya sakramenti zetu.
Hivyo tujitahidi kupambana na ugonjwa wa kukinai sakramenti na hakika tutaweza kupata msaada wa sakramenti zetu.
Katika somo la injili, Yesu anatupatia mfano wa mpanzi kuelezea namna jinsi tulivyoruhusu mioyo yetu kujifunua kuelewa ujumbe wa Mwenyezi Mungu. Hakika wapo ambao tangu mwanzo hawakulipatia nafasi neno la Mungu na mwishowe mbegu ilishindwa kuota au kuota na kukauka. Hii ni changamoto inayowapata wakristo wengi sasa. Hakika neno la Mungu halipatiwi nafasi na wengi wetu mbegu yetu inashindwa kuota au inaota na kunyauka mara moja. Sisi tuangalie ni kipi kinachotufanya tushindwe kumpatia Mwenyezi Mungu nafasi.
Urafiki mbaya, tamaa ya fedha, uasherati, unafiki, kusengenya au kukosa unyoofu vyote hivi vyaweza kuwa miongoni mwa vitu vinavyozuia mbegu ya imani kukua ndani mwetu. Lazima tuwe tayari kupambana na mambo haya.
Tumsifu Yesu Kristo
Maoni
Ingia utoe maoni