Ijumaa, Julai 16, 2021
Ijumaa, Julai 16, 2021,
Juma la 15 la Mwaka
Kut 11:10 – 12:14;
Zab 116:12-13, 15-18;
Mt 12:1-8
KUSHIKA SIKU TAKATIFU YA SABATO!
Karibuni sana ndugu wapendwa kwa adhimisho la Misa takatifu asubuhi ya leo.
Leo katika tafakari yetu ya Neno la Bwana, katika somo la kwanza, tunasikia juu ya ishara na maajabu aliyoyatumia Mwenyezi Mungu kusaidia kuwaondoa wana wa Israeli nchini Misri. Walipewa maagizo ya namna ya kufanya: ilibidi kumchinja Mwanakondoo na damu yake kupakwa juu ya miimo na vizingiti vya nyumba yao na kwa nguvu ya damu hii, waliweza kuokoka toka katika maangamizi ya yule malaika wa kifo aliyewaangamiza Wamisri. Ukisoma Kut 12:37, utagundua kwamba wapo ambao hawakuwa waisraeli ambao nao walikubali nyumba zao zipakwe hii damu na hakika waliweza kuokoka.
Twaweza kujiuliza, je hii damu ilikuwa ya namna gani? Ilikuwa na nguvu za namna gani? Hakika haikuwa tu na nguvu za damu ya mbuzi au kondoo wa kawaida bali ilikuwa na nguvu zaidi. Na nguvu hii ilipata toka kwa Mungu Mwenyewe. Na uwezo wa damu hii ulizidi kuonekana hata pale walipokuwa wanavuka bahari ya shamu. Ni wale tu walioshiriki katika kumla yule mwana kondoo na nyumba zao kupakwa hii damu ndio tu walioweza kuvuka. Wasiokuwa na hii damu waliishia kufa maji, walishindwa kuvuka kwenda upande wa pili.
Hakika damu hii ina nguvu ya pekee. Damu hii yaashiria ukuu wa damu ya Yesu. Hadi leo yeyote asiyefunikwa na damu hii hupotea, atashambuliwa na malaika wa mauti, na pia atashindwa kuvuka kwenda katika upande wa pili wa bahari yaani kwenye nchi ya ahadi mbinguni.
Sisi tuziheshimu sakramenti zetu. Tuepuke madharau. Hakika kwa macho zinaonekana kuwa ishara tu, lakini ndani yake zina neema kubwa, "supernatural grace".
Katika somo la Injili, Yesu anafundisha kwamba Sabato iliwekwa ili imsaidie mwanadamu, apate wokovu; na si ituletee chuki kati yetu. Kinachojenga ni upendo. Hata kama ni kwenye kushika sheria za Mungu, tuwe tayari kuangalia mazingira. Tusihukumu mtu fulani bila kuangalia nini kilichotokea, 'stress' alizokuwa nazo na mambo mengine mengi.
Tuwe na utayari wa namna hii. Tuache kufuata sheria bila kuonesha upendo.
Tumsifu Yesu Kristo.
Maoni
Ingia utoe maoni