Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumamosi, Julai 10, 2021

Jumamosi, Julai 10, 2021
Juma la 14 la Mwaka

Kumbukumbu ya Mtakatifu Bonaventure, Askofu na Mwalimu wa Kanisa

Mwa 49: 29-33, 50:15-25;
Zab 105: 1-4, 6-7 (R) Ps. 69:32;
Mt 10: 24-33.

MSIOGOPE

Ndugu zangu wapendwa, karibuni kwa adhimisho la misa takatifu. Neno la Bwana katika somo la kwanza, tunapewa habari juu ya kifo cha Yakobo na Yusufu. Wote hawa walikuwa watu wema walioifuata njia ya Bwana. Yusufu anasifika kwa tabia yake ya kuwasamehe ndugu zake kuepuka kuwatangazia kisasi ndugu zake. Jambo hili lilimfanya aendelee kubarikiwa na Bwana. Lakini pia liliwaletea fundisho ndugu zake kwani kama tunavyosikia katika somo la kwanza, wao walizidi kuhaha na kuwa na wasiwasi wakifikiria kwamba Yusufu atawalipiza kisasi. Lakini cha ajabu Yusufu hakutangaza adhabu.
Nasi tunaalikwa kumwiga Yusufu. Tutambue kwamba pale tutakapoepuka roho ya kisasi hapa ndipo chanzo cha sisi kubarikiwa zaidi. Na hapa tutaweza kutumika na Mungu kama vyombo vya kuwafundishia wenzetu hasa wale waliotutendea uovu. Lakini kama tutakuwa watu wa kurudisha visasi tutambue kwamba kwa hakika hatutaweza kutumika kama vyombo vya kuwafundisha wenzetu na Bwana. Tukubali kuacha roho ya kisasi na hakika tutaweza kuona baraka kubwa toka kwa Mwenyezi Mungu.
Katika somo la injili, Yesu anawapatia wafuasi wake ujumbe wa matumaini kwamba hakika hawapaswi kuogopa, wawe na tumaini kwa Mungu kwani hata nywele za vichwa vyao zimehesabiwa tayari. Huu ulikuwa ujumbe wenye lengo la kuwatia matumaini kwamba wasiogope mateso bali wamtegemee Mwenyezi Mungu. Hakika tumaini lao halitawahadaa, bali litawapatia uzima wa milele. Huu ndio upendo wa Mwenyezi Mungu kwetu. Hakika anaona kila kilicho chetu, mateso yetu na maumivu yetu yote anayaona. Sisi tuzidi kumtegemea Mwenyezi Mungu. Hakika atatuokoa na kutupatia ukombozi.
Pia anajua kila kitu. Hata kipindi cha mateso bado yupo nasi. Shetani ana lengo la kutuonesha kwamba sisi tumeachwa pweke. Hivyo anataka yeye aingie na kututawala. Ndivyo shetani alivyo. Lakini yafaa tutambue kwamba pale tunapojisikia kuwa wapweke sana ndio Mungu yupo karibu zaidi. Shetani lengo lake ni kutufanya tujisikie huo upweke na hofu ili basi tugeuke na kumfuata yeye. Tusikubali.

Maoni


Ingia utoe maoni