Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatano, Julai 07, 2021

Jumatano, Julai 7, 2021,
Juma la 14 la Mwaka

Mwa 41:55-57; 42:5-7, 17-24;
Zab 32:2-3, 10-11, 18-19;
Mt 10:1-7


IMANI YA MFUASI
Karibuni sana ndugu wapendwa kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana leo katika somo la kwanza tunakutana na tukio jinsi chuki na matendo yetu maovu yawezavyo kuwa sababu ya kuturudisha nyuma kimaendeleo.
Wana wa Yakobo walimuuza ndugu yao nchini Misri. Ndugu huyu (Yusufu) alikuwa na vipaji vingi, alikuwa na uwezo wa kupata maono mbalimbali na hakika baraka ya Mungu ilikuwa juu yake. Na kama hawa ndugu zake wangalimpokea na kushirikiana naye, kwa hakika wangekuwa mbali sana, wao wenyewe wangesaidika. Lakini cha ajabu hili liliwafanya wamchukie na hata kuamua kumuuza. Wanapomuuza, Mungu anazidi kumbariki; anakwenda kuvitumia vipaji vyake na baraka zake kwa watu wa taifa jingine.
Anaifanya Misri iendelee na Israeli irudi nyuma. Mwisho wa siku wanapata njaa na kwenda kuomba nchini Misri. Lakini ukisoma aliyesaidia kuiletea nchi ya Misri maendeleo na kuwa na akiba kubwa ya chakula ni huyu Yusufu aliyeuzwa na ndugu zake. Haya ndiyo yanayotokea hadi nyakati zetu. Wivu unatufanya tusiwe tayari kuwapokea wenzetu wenye ujuzi, tunaona wivu wa vipaji vyao vya uongozi, shuleni na katika jamiii. Mwisho wa siku tunadumaza maendeleo yetu wenyewe.
Baadhi ya wataalamu wanaweza wakakataliwa na sisi, labda kwa sababu ya chuki na hata kuwafukuza katika jamii yetu. Lakini mwisho wa siku wanakwenda kuleta maendeleo sehemu nyingine na mwishowe tunakwenda kuwa ombaomba kwao. Baadhi ya wataalamu walikataliwa katika nchi zao na kwenda kuleta maendeleo katika nchi nyingine. Mwisho wa siku tunakwenda kuomba msaada toka kwa hizi nchi. Lakini wataalamu wanaotumika ni wa kutoka katika nchi zetu hizi. Hivyo tujifunze sana kuondoa tabia za wivu. Wivu umezikosesha jamii zetu maendeleo. Wivu unatufanya turudi nyuma kimaendeleo. Tuondokane na tabia hizi.
Katika somo la injili, Yesu anawaita wanafunzi wake na kuwapa amri juu ya pepo wabaya na juu ya wagonjwa wote. Aliwaambia waanze na watu wa Israeli, wale waliokaribu kabisa kabla ya kwenda kwa watu wa mataifa. Waanze na nyumbani kwao kwanza, waimarishe nyumbani na ndio watoke nje. Nyumbani wakishindwa, basi ndio waende kwa watu wa mataifa. Sisi pia tunaalikwa kuiga walichoagizwa mitume. Yafaa tuanze na familia zetu, tuimarishe familia zetu kwanza kabla ya kwenda kwa wenzetu.
Viongozi yafaa waimarishe familia zao kwanza kabla ya kwenda kwa wenzao. Hii ni kwa sababu wengi wetu tunashindwa kusikilizwa pale tutoapo ujumbe kwa sababu hata kile tunachokihubiri hakifuatwi na watu wa nyumbani kwetu na mbaya zaidi hakifuatwi hata na sisi wenyewe. Yafaa tuanze kujihubiria sisi wenyewe kabla ya kwenda kwa wenzetu. Tumsifu Yesu kristo.

Maoni


Ingia utoe maoni