Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Alhamisi, Julai 01, 2021

Alhamisi, Julai 1, 2021
Juma la 13 la Mwaka

Mwa 22: 1-19;
Zab 115: 1-9;
Mt 9: 1-8


UJASIRI WAKUTAFUTA MSAMAHA

Ndugu zangu wapendwa, karibuni kwa adhimisho la Misa takatifu asubuhi ya leo. Neno la Bwana katika somo la kwanza, tunakutana na simulizi kuhusu utayari wa Abrahamu kumtoa Mwanae Isaka kama sadaka ya kuteketezwa. Hakika hili lilikuwa jaribu la ajabu kwani huyu ni mtoto wa pekee, aliyesubiri miaka 25 kumpata, na ambaye alikuwa ameahidiwa kwamba kwa njia yake uzao wake utaongezeka. Na pia Abrahamu alikuwa mzee tayari. Lakini haoneshi ugumu katika kukubali kumtoa mwanae kama sadaka.
Tukio hili lilimbariki kwa maisha yake yote. Likamfanya ndio uzao wake uongezeke na kuwa tukio la kusimuliwa kwa vizazi vingi. Tunachojifunza hapa ni kwamba ukarimu, utayari wa kutoa yote kwa ajili ya Mungu hakika ni ufunguo wa kupata yote. Mbele ya Mungu hakuna cha kupoteza. Kila unachokitoa kwa ajili ya Bwana, utashangaa hakitapotea-iwe ni muda wako, rasilimali zako. Tuondoe tabia yoyote ya kichoyo.
Abrahamu kadiri alivyozidi kujitolea kwa ajili ya Bwana, ndivyo alivyozidi na yeye kubarikiwa. Sisi tuwe tayari kuzifanya kazi ya Bwana. Tutoe rasilimali zetu kwa ajili ya Bwana. Pia tutoe muda wetu kufanya kazi ya Bwana. Juu ya Mlima wa Bwana, itapatikana neema, hivyo jitoe kwa ajili ya Bwana.
Mwenyezi Mungu alimzuia Abrahamu kumtoa Mwanae kama sadaka lakini Mungu Mwenyewe alikuwa tayari kumtoa Yesu Kristo Mwanae kama sadaka ya kuteketezwa. Tutambue kwamba Mungu anapokuambia tutekeleze sadaka kubwa, hakika ni yeye anayekuja kuitimiza sadaka ile. Yeye anakurudishia kama ilivyo –Yehova Yire. Juu ya mlima wa Bwana, hupatikana. Usiogope kujitoa kwa ajili ya Bwana, juu ya mlima wake, hakika atatoa.
Katika injili, tunakutana na habari za kupona Mwenye kupooza. Huyu mwenye kupooza anasaidiwa na rafiki zake, ndio wanaompeleka kwa Bwana. Imani ya walio karibu na mgonjwa inaleta uponyaji kwa mgonjwa. Hapa twajifunza umuhimu wa kuuguzwa na watu wenye imani. Watu wenye imani huleta uponyaji kwa wagonjwa. Lakini kuuguzwa na wasio na imani, ni sababu za wagonjwa wengi kupotea.
Sisi tunaotunza wagonjwa tujifunze kuwahudumia kiroho pia. Tuwapatie pia sakramenti za wagonjwa, tuwapatie sakramenti ya upatanisho na Ekaristi. Hizi huwaponya kiroho na kimwili. Tusiache kutumia sakramenti hizi.

Maoni


Ingia utoe maoni