Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Ijumaa, Julai 02, 2021

Ijumaa, Julai 2, 2021,
Juma la 13 la Mwaka

Mwa 23:1-4,19, 24:1-8,62-67;
Zab 105: 1-5;
Mt 9: 9-13

MDHAMBI ANAKARIBISHWA KWA HURUMA

Ndugu zangu wapendwa, karibuni kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Leo katika tafakari ya neno la Bwana, katika somo la kwanza, Abrahamu anapoteza mke wake kipenzi ndiye Sara. Tukio hili linakuwa la uchungu sanaa kwake lakini yeye analipokea kwa utulivu na imani na kumzika mke wake. utulivu wake unaonesha ukuu wa imani ya Abrahamu. Matatizo haya hayamfanyi aanguke kiimani.
Ndugu zangu, Abrahamu atupatie somo hasa sisi wakristo. Nyakati za matatizo zitatupata. Wakati mwingine tunayumbishwa na vipindi vya matatizo na uchungu na kutufanya tupoteze imani. Hivi havifai kutuyumbisha ndugu zangu. Tukumbuke kwamba nyakati za shida zitatokea, nyakati za matatizo makubwa zitajitokeza katika maisha. Lakini tunapaswa kumuiga Abrahamu. Tuoneshe utulivu mkubwa. Moyo uliojaa utulivu ni dhihirisho la ukuu wa imani yetu.
Katika injili, Yesu anamchagua mtoza ushuru, Matayo kuwa mfuasi wake. Mfuasi huyu kwa mwanzoni hakupokeleka na wengi kwa sababu alikuwa mtumishi katika serikali ya kirumi-serikali iliyochukiwa na Wayahudi kwa kiasi kikubwa kwani ilionekana kuwa serikali dhalimu. Hivyo Matayo alionekana kuwa msaliti, aliyeitumikia serikali ya kikoloni. Pia kwa kipindi hicho, watoza ushuru wengi walikuwa wala rushwa kwani walitoza kingi zaidi ya kilichoagizwa. Jambo hili liliwachafua sana na kuonekana kuwa watu wachafu. Lakini Bwana Yesu anakuwa tayari kumchagua huyu kuwa mfuasi wake.
Hakika Matayo alipewa heshima na upendeleo wa pekee na alipaswa kuupokea upendeleo huu kwa heshima kubwa. Na hakika alipokea upendeleo huu vyema. Sisi tutambue kwamba upo wakati Bwana Yesu anatuletea nafasi ya upendeleo, hasa wakati tunapokuwa katika dhambi zetu. Yeye atajitokeza na kutoa nafasi ya upendeleo. Hata kama mtu ni mbaya kiasi gani, tutambue kwamba upo wakati Bwana Yesu atatuletea nafasi ya upendeleo.
Yafaa tujifunze kuzipokea nafasi hizi vyema kama alivyofanya Matayo: Matayo aliacha kazi yake na kumfuata, alipata upendeleo na kuacha matendo yake maovu. Nasi tufanye hivyo hivyo. Nafasi ya upendeleo tuipatapo, tukubali kuacha matendo yetu ya giza na kumfuata Bwana. Wengi tunaanguka kwa sababu hatujajifunza kupokea nafasi hizi za upendeleo vyema. Tujitahidi.

Maoni


Ingia utoe maoni