Alhamisi, Juni 10, 2021
Alhamisi, Juni 10, 2021.
Juma la 10 la Mwaka
2 Kor 3:15 – 4:1,3-6;
Zab 85:9-14;
Mt 5:20-26
KUFANYA MAKAO!
Karibuni sana wapendwa wangu kwa adhimisho la misa takatifu asubuhi ya leo. Leo tafakari yetu inaanza kwa kuiangalia Zaburi yetu ya wimbo wa katikati. Zaburi hii inatupatia ujumbe kuhusu Utukufu wa Bwana kukaa kati yetu. Matunda ya utukufu wa Bwana kukaa kati yetu ni kuwa na amani, furaha na upendo kati yetu. Bwana huwa karibu nasi naye hutupatia msaada.
Katika Somo la kwanza, Mt. Paulo anaeleza kwamba Wayahudi waliokataa kumtii Kristo walishindwa kuukaribisha utukufu wa Mungu uje ukae kati yao. Hivyo walibakia katika upofu, akili zao zikafunikwa na giza. Giza hili litaondolewa kwa pale watakapomgeukia Kristo na kuiamini injili yake. Ndugu zangu, Wayahudi wanaelezwa kwamba ipo faida kubwa ikiwa wataipokea injili. Injili itawaletea ukamilifu. Injili itawapatia uhuru na kujua namna ya kuenenda kati kati ya ulimwengu huu.
Wakristo wa Mwanzo waliporuhusu injili iwaongoze, walipata amani kubwa maishani mwao. Japokuwa walikuwa watu wa kipato cha chini, waliweza kuishi maisha ya uhuru na kutokutindikiwa. Injili ilimgusa kila mkristo ili aweze kumsaidia mwenzake. Kila aliyeeleza shida yake aliweza kusaidiwa kwa sababu injili iligusa maisha yao. Na hivyo walipoelezana shida, walisikilizana. Hivyo kanisa liliweza kukua sana.
Sisi tuzidi kukazana kuishi injili yetu. Nyakati zetu, wengi wetu tunapata shida kwa sababu wengi hatuguswi na injili. Hivyo hata wenzetu wakitueleza shida zao, hatusikilizi. Yafaa injili itusaidie, tubadilike tena.
Katika somo la injili, miongoni mwa yanayofundishwa na Yesu ni juu ya kutambua kwamba hawapaswi kujilinganisha na wafarisayo au wanasheria. Maisha yao ya kimaadili yanapaswa kuwapita hata ya hawa wafarisayo. Yesu anawataka wawe watu wenye kutoa vitu vyenye ubora. Hata sadaka zao na sala zao mbele ya Mungu zafaa ziwe bora. Wazitoe katika moyo safi, baada ya mapatano na wenzao, hapa Mungu atazipoke. Huu ndio ukristo.
Injili hii iwe fundisho kwetu ndugu zangu. Mara nyingi, wengi wetu hatukui kimaadili kwa sababu tunatabia ya kujilinganisha na wenzetu. Tunajilinganisha na wezi, wauaji na kusema labda sisi ni bora kuliko wao. Na hivyo tunakuwa tayari kusema kwamba afadhali hata mimi natendaga dhambi ndogo. Wenzangu wanatenda zaidi. Na hivyo tunahalalisha dhambi zetu na mwishowe tunaanguka kiroho. Hii sio sahihi.
Tunapaswa kujua kwamba kama ni wema, tuwe na wema wa hali ya juu kabisa. Tuache kuhalalisha dhambi kwa kujilinganisha na wenzetu. amina.
Maoni
Ingia utoe maoni