Jumanne, Mei 25, 2021
Jumanne, Mei 25, 2021
Juma la 8 la mwaka wa Kanisa
YbS 35: 1-12;
Zab 50: 5-8;
Mk 10: 28-31.
KUMFUATA YESU BILA MASHARTI!
Karibuni ndugu zangu wapendwa kwa tafakari ya neno la Mungu katika adhimisho la Misa Takatifu. Leo miongoni mwa ujumbe tunaopewa na Yoshua bin Sira ni kufanya urafiki na Mungu kwa mali ya dunia tuliyonayo. Chochote ulichopewa na Mungu-hata kama ni uwezo wako wa kiakili, ujuzi mzuri, fedha, uwezo wa kueleza na kufafanua mambo, lazima tuutumie kuanzisha nao urafiki na Bwana. Tuwe wakarimu katika kuanzisha urafiki huu, hata kama ni cheo chako na madaraka yatumie vizuri wakati huu kuanzisha urafiki na Bwana.
Tumia ujuzi wako, kazi yako ofisini, tuwe tayari kuanzisha urafiki huu na hakika tutafanikiwa mnoo. Usikubali nyumba ya Mungu ibaki mahame wakati wewe unakaa sehemu za kungaa na za hali ya juu, toa michango na kujitoa kuhakikisha sehemu ya Mungu ni nzuri, usikubali nyumba ya rafiki yako ( Yesu alituita rafiki) iwe mahame, itunze na lijali kanisa zaidi na zaidi. Tutafanikiwa sana.
Lakini wengi wetu-kadiri tunapopata mali urafiki wetu na Mungu unapotea polepole, tunapatwa na kiwewe cha kutenda uovu na kutufanya tukosane na Mwenyezi Mungu. Wapo wanaotumia umaarufu wao au uzuri wao au fedha zao kutenda uovu. Hii ni sababu ya wengi kunyanganywa nafasi walizopewa na Bwana. Tutambue uchoyo kwa Mwenyezu Mungu ndicho chanzo, mwanzo wa wengi wetu kuanguka. Tujitahidi kuondokana na uchoyo mbele ya Mungu.
Katika somo la Injili Yesu anadhihirisha kwamba aliyemkarimu kwa Bwana hupokea zaidi. Anawaeleza wanafunzi wake kwamba kama watakuwa tayari kujitoa kwa Bwana, hakika watapokea mara mia, sisi tuzidi kuwa wakarimu kwa Bwana. Wengi wamebarikiwa kwa ukarimu kwa Bwana. Wapo wachoyo wanaoficha vitu lakini hawaendelei, kila siku wanarudi nyuma licha ya kuficha na kujikusanyia. Tuwe tayari kutoa muda wetu kwa sala, kusaidia maskini, na kufanya shughuli zetu, hapa ndipo tutakapo barikiwa. Tuwe wakarimu wa kutumia nguvu zetu, vipaji vyetu na vyeo vyetu kumtangaza Bwana. Tuache uchoyo.
Maoni
Ingia utoe maoni