Jumatatu, Mei 17, 2021
Jumatatu, Mei 17, 2021.
Juma la 7 la Pasaka
Mdo 19: 1-8;
Zab 67: 2-7 (R. 33);
Yn 16: 29-33.
WAKRISTO WENYE KUTOA USHUHUDA!
Karibuni sana ndugu zangu wapendwa kwa tafakari ya neno la Bwana asubuhi ya leo katika adhimisho la Misa Takatifu. Leo neno la Bwana linaanza kwa kulitazama somo la kwanza. Hapa tunakutana na Mtume Paulo akiwaombea Roho Mtakatifu wafuasi wa Kristo huko Efeso. Wafuasi hawa walibatizwa na Apolo kwa ubatizo wa toba, wa Yohane Mbatizaji.
Paulo anawawekea mikono na kupokea nguvu ya Roho Mtakatifu na kuanza kuongea kwa ndimi. Roho Mtakatifu alihitajika ili kuwaimarisha wafuasi hawa ndugu zangu. Bila huyu Roho Mtakatifu, wasingaliweza kuiishi imani yao. Yesu aliwaagiza wafuasi wake kwamba wasijaribu kutoka Yerusalemu kabla ya kumpokea Roho Mtakatifu. Pale wangejaribu hivyo, wasingaliweza kumtangaza Kristo, kwanza wangekosa maarifa ya kumtangaza kristo, halafu wangekosa cha kutangaza, na wangekosa nguvu ya kutangaza. Hivyo, wangalishindwa kirahisi. Hivyo, ilibidi wampokee Roho Mtakatifu ili waweze kupokea haya.
Leo Paulo anawaombea Roho Mtakatifu ili wakristo wa Efeso waweze kuishi imani yao hivi, na kupata cha kutangaza na kuweza kumtangaza Kristo wetu vyema. Sisi tujifunze kutambua nafasi ya Roho Mtakatifu maishani mwetu hasa katika imani yetu. Tukijiona tunatetereka kiimani, tunaanguka kirahisi, tunakuwa waoga, tunakosa hekima ya kuongoza maisha yetu, tunafungwa na ulevi, uasherati, na fujo-tukiona haya-lazima tuchunguze uhusiano wetu na Roho Mtakatifu. Tunapaswa kumwalika Roho atusaidie kwani ndiye atakayetusaidia katika magumu ya namna hii ndugu zangu.
Yesu katika injili anatueleza kwamba ulimwenguni tutapata magumu lakini tujipe moyo. Sisi tusiache kujipa moyo, tuna kila sababu ya kujipa moyo kwani tunaye Roho Mtakatifu. Hakika atatusaidia. Yesu aliweza kushinda. Nasi tusiache kujikabidhi mikononi mwa Roho Mtakatifu. Hakika tutashinda. Tuzidi kujiombea wenyewe, tuwaombee na ndugu zetu na viongozi wetu, ili wazidi kupokea baraka toka kwa Mwenyezi Mungu, na Roho wa Mungu aongoze mawazo yao na utendaji wao. Tumsifu Yesu Kristo.
Maoni
Ingia utoe maoni