Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Alhamisi, Machi 04, 2021

Alhamisi, Machi 4, 2021.
Juma la 2 la Kwaresima

Yer 17:5-10;
Zab 1:1-4, 6;
Lk 16:19-31

UPENDO WA MUNGU KWA MASKINI

Karibuni ndugu zangu wapendwa kwa adhimisho la Misa Takatifu Asubuhi ya leo. Leo neno la Bwana katika somo la kwanza tunakutana na Nabii Yeremia akitoa unabii-anasema kwamba amelaaniwa yule amtegemeaye mwanadamu, amfanyaye Mwanadamu kuwa sababu yake yeye kujiona salama, na kumtupia matumaini yote. Huyu hatadumu na kusonga mbele, kwani ni kama mti uliooteshwa jangwani, pasipo na maji, au juu ya chumvi pasipo na rutuba yoyote-na hakika hawataweza kuendelea, utanyauka tu, utatumia nguvu nyingi bila mafanikio yoyote. Wataishi kwa kupoteza muda na rasilimali zao.
Ujumbe huu ulielekezwa na Yeremia kwa wana wa Yuda-wao waliacha kumtegemea Mungu awapatie ulinzi dhidi ya mashambulizi toka taifa la Wababuloni-waliishia kulitegemea taifa la Misri liwaokoe. Yeremia anawaeleza kwamba huku kuitegemea Misri kutawaletea laana-watapoteza rasilimali zao na muda wao na mwishowe watapoteza hata miji na hekalu na maisha ya wengi. Haya yaliyotabiriwa na Yeremia yaliwatokea wana wa Yuda kama ilivyokwishatabiriwa.
Somo hili litupatie fundisho. Litukumbushe jinsi tulivyokwishapoteza muda, rasilimali, afya na hata uhai wa wenzetu kwa sababu ya kutokumtegemea Mungu na kutegemea nguvu zetu. Wengi wetu ni maskini sasa na baadhi wamepoteza uhai kwa sababu ya kumtupa Mungu pembeni. Tumwalike Mungu kati yetu kwa kila jambo. Tuanze kila kitu kwa sala, pia tushukuru baada ya kupokea toka kwa Mungu. Hapa itatufanya tufaidi zaidi.
Tajiri tunayemsikia katika injili aliishi kwa kutegemea nguvu zake, alijilimbikizia vyakula vingi mwenyewe na kukataa kumshirikisha Mungu amwandalie maisha yake ya baadaye. Mwishowe anakaribishwa kwenye Jehanamu na kila alichokifanya ulimwenguni kiliishia kuwa bure, alipoteza muda wake na nguvu, na mali zake alipokuwa ulimwenguni. Hazikumsaidia chochote kwa maisha ya baadaye. Alipaswa kumshirikisha Mungu.
Sisi tumshirikishe Mungu kwa kila tufanyalo maishani. Hakika tutafaulu sana. Tusali kupata chakula chetu, kuombea masomo yetu, magonjwa yetu na afya zetu. Hakika tutaepuka kupoteza muda na rasilimali. Tumsifu Yesu Kristo.

Maoni


Ingia utoe maoni