Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatano, Februari 17, 2021

Jumatano, Februari 17, 2021
Jumatano ya majivu (Siku ya kufunga na kujinyima)

Yoel 2: 2-18;
Zab 51: 3-17;
2 Kor 5:20 – 6:2
Mt 6: 1-6, 16-18
KUTOKA MAJIVU MPAKA KWENYE UTUKUFU!

Leo tumeanza kipindi cha neema cha Kwaresima, na tunaitwa kusali, kutolea sadaka na matendo ya huruma. Tukiwa tunatafakari kipindi hichi, tukiangalia mbele katika kuadhimisha mateso, kifo na ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo. Maisha ya toba na kuongoka ndio maada kuu ya Kwaresima.
Katika somo la kwanza ujumbe wa wongovu umetengenezwa na maneno haya “mrudieni Mungu kwa mioyo yenu yote” (Yoel 2:12). Kwa Yoeli, kuongoka ni njia ya kurudi nyuma. Wale wote waliojiweka katika njia isio sawa wanaitwa kurudi nyuma. Katika somo la pili Paulo anaongelea kuhusu upatanisho. Anasema “tunaomba Mungu awapatanishe” upatanisho na Mungu unapatikana kwa kuishi ujumbe unaoletwa kwetu na wajumbe wa Mungu-wajumbe waneno lake (Warumi 10:14, 17).
Katika somo la Injili Yesu anaongelea mara saba tuzo ambalo wanalipokea wale wanaotenda kadiri ya mafundisho yake. Injili mara nyingi inaelezea kuhusu ‘tuzo’ walilowekewa wenye haki na ‘adhabu’ kwa walio waovu. Tuzo analo liongelea Yesu, sio kuwa na sehemu nzuri ya juu mbinguni bali , kuongezeka mapendo, hali ya muunganiko wa ndani, na hali ya kufanana na uso wa Baba wa mbinguni. ‘Tuzo’ ni furaha ya upendo wa hali ya juu, kama Mungu anavyofanya, ni hali ya “kuwepo katika ufalme wake”. Kukuwa katika hali hii ya juu, katika mwanzo wa kwaresima Yesu anatualika tufanye mambo matatu: kutolea sadaka, sala na kufunga. Hizi zinajenga nguzo tatu za kiroho za Wayahudi, na yeye anaziweka tena lakini katika hali yake ya kipekee.
Sadaka: katika kipindi cha Yesu, baadhi ya watu walikuwa wana jukumu la kukusanya na kugawa sadaka kwa maskini, yatima, wajane na wasio jiweza. Wakati wa Sabato, kulikuwa na tabia ya kuwasifia wale waliotoa nyingi na walitangazwa mbele ya mikusanyiko. Kwa Yesu, kutoa sadaka sio kuweka hela kidogo, bali kuwa na haki, ni kutambua kuwa vitu vyote vya dunia sio vyetu ni vya Mungu. Kil aliyechukuwa zaidi anapaswa kurudisha kwa wale wasio nacho. Mt. Ambrose, aliwaambia matajiri “kumbuka kwamba, hamuwapi maskini kilicho chenu; bali mnawapa tu kile kilicho mali yao”
Sala: wakati wa kipindi cha Yesu kulikuwa na aina mbili za sala: sala ya pamoja na sala binafsi. Sala za pamoja, zilifanywa hekaluni, katika masinagogi na katika mitaa, mara mbili kwa siku. Yesu hakatazi matendo haya. Yeye anaelekeza macho yake zaidi kwenye sala ya binafsi, ambayo inafanywa na mtu mwenyewe, milango imefungwa katika hali ya muunganiko wa ndani na Baba “anaye ona vyote”. Sala hii sio marudio ya fomula mbali mbali, bali ni mazungumzo na Mungu, nikumwomba asikilize mapenzi yetu na kutimiza ndoto zetu, lakini pia kuishi mapenzi yake na kupokea kutoka kwake majukumu aliotupangia ya kujenga ufalme wake. Sala, kwanza kabla ya yote ni kusikiliza, kufungua mioyo yetu na kukaribisha mipango ya Mungu na bila kukiuka matazamio yake.
Kufunga: katika kipindi cha Yesu, waliamini kwamba kufunga kwa kweli ilileta baraka kubwa sana: ilisaidia kuacha dhambi, na kumfanya Bwana aone huruma, kuepuka adhabu yake, na kukinga na mabaya yote. Kufunga kwa Mkristo haihitaji kutambulika. Wanaosha nyuso zao na kuonekana wenye furaha, ana furaha kwasababu kwa kujinyima kwake anamuona maskini akifurahia kutumia ulichompa. Kufunga kuliko kubalika na Mungu ni “kuvunja aina zote za ukosefu wa haki….funga kwa kushirikisha mkate wako na wale walio na njaa, walete katika nyumba yako wasio na nyumbani, wavalishe wale walio uchi” (Isa 58:6-7). “kuweni wakarimu kati yenu …msiweke maovu juu ya mwingine ndani ya moyo yenu” (Zek 7:5-10).
Katika mwanzo wa kwaresima tunakumbushwa kwamba Kwaresima inaanza na majivu na kuishia na moto, moto wa pasaka wa ufufuko na moto wa Roho Mtakatifu wakati wa Pentekoste, uhakika wa jinsi tutakavyo kuwa. Yesu amezamisha uwepo wetu ambao ni vumbi na majivu katika damu yake, na kutuwezesha kufufuka katika maisha mapya. Roho Mtakatifu anatufanya viumbe vipya.

Sala:
Bwana, ninaomba kwaresima hii iwe yenye matunda katika maisha yangu. Ninaomba kiwe kipindi cha neema cha kukumbatia yote unayotaka niyafanye ndani yangu. Yesu, nakuamini wewe.
Amina

Maoni


Ingia utoe maoni