Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatatu, Februari 15, 2021

Jumatatu, Februari 15 2021
Juma la 6 la Mwaka wa Kanisa

Mwa 4: 1-15, 25;
Zab 50: 1, 8, 16-17;
Mk 8: 11-13

MIUJIZA KUTOKA MBINGUNI!

Karibuni ndugu zangu wapendwa kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo neno la Bwana linaanza kwa kuiangalia Zaburi yetu ya Wimbo wa katikati toka zaburi ya 50. Hapa tunakutana na Zaburi isemayo: umtolee Mungu dhabihu za kushukuru. Hii ni amri, zaburi hii inasisitiza pia tena kwamba kila tujapo kwa Bwana kwa ajili ya hii dhabihu, lazima moyo wetu uwe safi. Na hapa Bwana huipokea na kuibariki dhabihu hii.
Leo katika masomo yetu, anayetimiza hili ni Abeli. Yeye anakuja mbele ya Bwana na dhabihu ya kushukuru, na anakwenda na moyo safi, na dhabihu yake inakubaliwa. Kaini anakwenda na moyo mkaidi, na mara moja inakataliwa. Moyo wa uchoyo na hasira na chuki ndio unaofanya dhabihu nyingi zisikubalike. Yawezekana Kaini alikwenda mbele za Bwana na moyo kama huu. Bwana hakupokea dhabihu yake. Sisi tutambue kwamba ni wajibu wetu kutoa dhabihu mbele ya Bwana. Sisi tuje mbele ya Bwana, tuondoe chuki, na hasira na uchoyo. Uchoyo unaotukumba wengi ni kukataa kutoa mUda Wetu kwa Bwana.
Kuna wakati kweli tunanogewa na kazi, kazi inanoga tunamtupa Bwana pembeni. Pia tunakuja na chuki sana na wengine-mbele ya Yesu hakuna haja ya kuhifadhi chuki kabisa. Huu ndio udhaifu wetu, lakini inatupasa kuuleza mbele ya Bwana, tuukubali udhaifu huu. Tumuombe atusaidie.
Kwenye somo la Injili, Yesu anakataa kuwapatia ishara Wafarisayo. Yesu anakataa kuwapa ishara kwani hii ilikuwa ni ishara kwa wasio na Imani, walitaka kumjaribu. Kati ya vitu anavyovichukia Yesu ni kutaka kujaribiwa. Yeye anatenda muujiza kwa aliye na imani. Hata siku moja hatendi muujiza kwa asiye na imani. Hiki kilichowapata mafarisayo ndicho kinachotutokea na sisi kila siku ndugu zangu. Wengi wetu hatujibiwi kwa sababu tunakwenda mbele ya Yesu bila imani.
Ukosefu wa unyofu unatukosesha mengi, tukiwa mbele ya Yesu ni lazima tuoneshe unyofu. Yesu alisema heri walio wanyofu wa moyo, maana watamuona Mungu. Unyofu wa moyo ni kuishi kiapo chako bila kuonesha ufarisayo, bila kuwa ndumila kuwili, kama ni watu wa ndoa tunaishi kama watu wa ndoa kweli. Sisi tukazane kuwa wanyofu. Unyofu ni ufunguo wa baraka maishani mwetu.

Maoni


Ingia utoe maoni