Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatano, Februari 10, 2021

Jumatano, Februari 10, 2021
Juma la 5 la Mwaka

Mwa 2: 4-9, 15-17;
Zab 103: 1-2, 27-30;
Mk 7: 14-23.

NDANI NA NJE!

Ndugu zangu karibuni kwa tafakari ya neno la Bwana asubuhi ya leo katika adhimisho la Misa Takatifu. Tafakari yetu inaanza kwa kuiagalia zaburi yetu ya wimbo wa katikati. Hapa tunamkuta mzaburi akifurahia uumbaji na kuusifu. Anatangaza kwamba viumbe vyote vimeumbwa na Bwana na vyote ni lazima vimwangalie Bwana ili apate kuvilisha. Mungu asipofungua mikono yake hakika hivi haviponi. Mwanadamu ameumbwa ili amwangalie Bwana.
Ndio ujumbe tunaoukuta tena katika somo la kwanza ambapo tunasikia habari juu ya uumbaji wa mwanadamu. Yeye anapoumbwa, anapatiwa maagizo maalum, kwamba ale matunda ya miti yote lakini mti maalumu alioambiwa na Mungu asile matunda yake. Hili lilikuwa agizo la kiutii, kwamba Mwanadamu alipaswa kumuangalia Mungu apate kumlisha. Hivyo alipaswa kula kile alichoagizwa na Mwenyezi Mungu.
Sisi ndugu zangu tutambue kwamba tunalishwa na Mwenyezi Mungu. Hivyo ni lazima tumtazame yeye kila siku ili apate kutulisha. Wengi wetu hatujui kumtazama Bwana na ndio maana tunaishi katika njaa. Mwanadamu analishwa na Bwana. Na wakati tunalishwa na Bwana, lazima tufuate masharti-yeye aliwaambia wazazi wetu wa mwanzo wasile matunda ya mti wa katikati. Sisi tunaugua kwa sababu ya kula vilivyokatazwa. Wengi wetu tunateseka sasa, tunakazana kutoa sumu mwilini, wengine wamepoteza uhai kwa sababu ya kutokufuata masharti. Tuwe watu wa kufuata masharti na tuwe na utii.
Katika injili yetu, Yesu anaendelea kuwapinga wafarisayo na waandishi juu ya sheria zao za kutawadha na za vyakula. Anasema kwamba kile kinachomuingia mwanadamu hakiwezi kumfanya najisi, ni kile kimtokacho.
Wafarisayo walipotoka kwa sababu walijali sana kile kilichoingia kuliko kilichotoka moyoni mwao. Labda waliona afadhali kumdhulumu jirani kuliko kula na mikono isiyotawadhwa, au walikuwa tayari kumtelekeza mgonjwa kuliko kumgusa na kujisababishia unajisi. Tabia za namna hii ziliwakosesha mbingu. Sisi tusiwe kama wafarisayo. Wapo baadhi yetu tulio tayari kutoa michango mikubwa kanisani lakini nyumbani mwetu wapo mayatima au majirani maskini na hatuko tayari kuwasaidia. Tuwe watu wa kiroho, wenye kuongozwa na huruma. Tuache kutenda matendo ya nje ili tuwafurahishe wengine. Sisi tupanie kumfurahisha Bwana.

Maoni


Ingia utoe maoni