Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumanne, Februari 02, 2021

Jumanne , Februari 2, 2021,
Juma la 3 la Mwaka wa Kanisa

Sherehe ya Kutolewa Bwana hekaluni.

Mal 3: 1-4;
Zab 24: 7-10;
Ebr 2: 14-18
Lk 2: 22-40.

KUJIWEKA WAKFU KWA BWANA!

Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo tunaadhimisha siku ya kutolewa Bwana hekaluni. Hii ilikuwa ni desturi katika tamaduni za Kiyahudi kwamba mtoto wa kiume aliyekifungua mimba lazima aitwe mtakatifu wa Bwana. Anatolewa ili awe mali ya Bwana, awe chombo cha Bwana, amtumikie Bwana na si shetani. Hadi leo katika kanisa wazo hili linapendelewa sana na hadi leo tunashuhudia watawa wakijitolea mbele ya Bwana na leo ni siku yao. Wao huiga mfano wa Yesu, kuyatolea maisha yao kwa ajili ya Bwana na kufanya kazi yake. Hivyo, leo tuwaombee watawa wetu ambao kwa kweli wamechagua kufuata wazo na fungu jema. Nasi ndugu zangu, tunaalikwa kuyatolea maisha yetu yote kwa ajili ya Bwana. Haya ndiyo mawazo makuu yanayotuongoza katika siku ya leo ndugu zangu.
Na tukianza kwa kuyachunguza masomo yetu ya leo, tunaona wazo hili la kuwekwa wakfu, wazo la kutakaswa limejitokeza vizuri kabisa. Somo la kwanza linatoka katika kitabu cha nabii Malaki ambaye analijia hekalu. Cha ajabu ni kwamba mjumbe huyu anapofika, sio kwamba hekalu linamtakasa bali ni hekalu lenyewe linapata kutakasika na dhabihu zinazokuwa zinatolewa pale zinatakaswa na kupatiwa ubora zaidi. Katika Injili, tunagundua kwamba mjumbe huyu sasa amekwisha zaliwa, ambaye ndiye Yesu na leo sasa anapelekwa hakaluni kutakaswa. Na anapofika hekaluni, hakalu linapata baraka badala ya hekalu kumpatia Baraka. Zile sadaka zinazokuwa zikitolewa hakaluni zinapatiwa ubora, Mungu mwenyewe anazipatia kiwango, furaha inazidi kwa Mungu kuja hekaluni, na dunia yote inabarikiwa. Hekalu lenyewe linawekwa wakfu. Katika somo la pili tunasikia kwamba Yesu analiweka wakfu, sio hekalu peke yake bali amekuja kuwaweka wakfu watu wote, watu wote kabisa, wanaomwamini kwa damu yake sasa wanakombolewa.
Ndugu zangu, ndivyo ilivyo kwa siku ya leo. Leo tunaambiwa kwamba Yesu amekwisha kufika. Ujio wake tu tayari umetutia wakfu. Anapofika hekaluni, hekalu halimweki wakfu bali yeye ndiye analiweka . Sasa, anapofika kwetu, vivyo hivyo anatuweka wakfu kwa njia ya sakramenti mbalimbali. Basi, tuishi kama tuliowekwa wakfu. Tuachane na kuitumia miili yetu vibaya, tuwasaidie na wengine waweze kujitoa wakfu kwa Bwana. Ukimuona mwenzako anakataa kuishi utakatifu, msaidie, usimletee vishawishi au kumshauri vibaya.
Tujue kwamba ni dhambi kubwa kumfanya mwenzako anayetaka kujiweka wakfu aidha kwa kuishi kiaminifu ndoa yake au utawa wake, sasa wewe unamdanganya asiiishi kiwakfu. Kama umeshafanya hivyo ungama. Popote pale ambapo umewahi kumfanya mwenzako ashindwe kuishi kiwakfu, asiyaishi maisha yake kitakatifu tujirekebishe.
Kuwashawishi watu waliojiweka wakfu aidha kwa ndoa takatifu au utawa na kuwadumbukiza ufanye nao dhambi au kwa kushirikiana nao na wewe ukawapeleka katika dhambi kama kushiriki katika rushwa Fulani, ukawafundisha uzinzi, jua ni dhambi kubwa. Ni kama mtu mwenye kuikufuru madhabahu ya Bwana. Hivyo, tuwe makini. Ogopa kitu kilichotolewa wakfu kwa Bwana. Kitakulaani maisha yako yote.

Maoni

DISMAS KIMVULE

Ni tafakari nzuri

Ingia utoe maoni