Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Ijumaa, Januari 29, 2021

Ijumaa, Januari 29, 2021,
Juma la 3 la Mwaka wa Kanisa

Ebr 10: 32-39;
Zab 37: 3-6, 23-24, 39-40;
Mk 4: 26-34

MBEGU ZA UFALME WA MUNGU!
Ndugu zangu karibuni kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo.Wokovu wa wenye haki watoka kwa Bwana. Huu ni ujumbe wa zaburi yetu ya wimbo wa katikati. Inasisitiza kwamba Bwana humlinda mwenye haki, humpatia wokovu. Wokovu wa yeyote mwenye haki upo kwa Bwana.
Hivyo mzaburi anawatia moyo waamini wazidi kumwamini Bwana. Hakika hatawaacha bila kuwakumbuka. Zaburi hii inatumika kutilia mkazo ujumbe wa somo la kwanza ambapo mwandishi wa barua kwa Waebrania anawaeleza kwamba yawabidi wabakie katika imani. Wao ni watu wa imani na kuna kipindi kilipowabidi kuteseka kwa sababu ya imani yao. Hili lipo lakini hakika Bwana hatawaacha. Hivyo wasikatishwe tamaa na maumivu au masengenyo wanayoyapata. Bwana atawakumbuka na hataacha kuwapatia wokovu.
Ujumbe huu ututie moyo na sisi ndugu zangu kwamba ipo siku tutafurahia pamoja na Bwana-ipo siku machozi yetu na maumivu yetu, mahangaiko na wasiwasi wetu zitafikia mwisho. Ipo siku. Hivyo tujipe moyo. Wale tulio wagonjwa tufarijiwe na neno hili. Na wale tunaowatunza wagonjwa wetu pia tufarijiwe na neno hili. Litufariji na baadhi yetu pia ambao tunafanya kazi zenye kuchosha kweli kiasi kwamba miili yetu hubakia hoi kila siku. Tufarijiwe na neno hili.
Kwenye somo la injili, Yesu anaelezea ufalme wa mbinguni kama ufalme ambao upo ili ukue-na si udidimie. Upo kwa ajili ya watu, na unasubiria watu wajiunge ndani. Mfano wa kwanza unatuambia kwamba ufalme huu tayari una nyenzo zake za kuufanya ukue. Kila nguvu na neema zipo ndani yake. Ni juu yam mea au mwanadamu kutumia vile virutubisho vilivyoko. Sisi wakristo tutumie sakramenti zetu vyema na viongozi wetu ili tupate kukua.
Mfano wa pili unaonesha kwamba ufalme huu huanzia katika mambo madogo na kuishia kuwa makubwa. Yote haya yanawezekana kutokana na neema ipatikanayo ndani ya ufalme huu. Sisi tushirikiane na neema iliyo ndani ya huu ufalme na hakika tutafika mbali. Katika udogo wetu na umaskini wetu-tukishirikiana na Bwana, twaweza kufanya makubwa. Tuache tabia za kusingizia umaskini na mwishowe kuishia bila kufanya chochote. Huku ni kuchezea neema ya Bwana.
Hakuna aliyepewa kidogo sana ambacho Mungu hajalenga kiwe kikubwa. Sisi tusikubali kudumaza yale madogo aliotupatia Mungu. Anatuhitaji tuyakuze kwa maisha yetu na kuwa makubwa kwa kujenga ufalme wake.

Maoni


Ingia utoe maoni