Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumamosi, Januari 16, 2021

Jumamosi, Januari 16, 2021,
Juma la 1 la Mwaka wa Kanisa

Ebr 4: 12-16;
Zab 18: 8-10, 15;
Mk 2: 13-17

KUMLETA YESU KWA “WASIOMTAMANIKA”!

Karibuni sana ndugu zangu kwa tafakari ya neno La Mungu asubuhi ya leo katika adhimisho la Misa Takatifu. Leo tafakari yetu inaanza kwa kuiangalia zaburi yetu ya wimbo wa katikati na hapa tunakutana na ujumbe usemao: neno lako ee Bwana ni roho na uzima.

Neno hili linauwezo wa kumtia mjinga hekima. Na hakuna yeyote mwenye kuyatii maneno na kupotea. Ni lazima yatamuokoa tu. Somo la kwanza linaendeleza ukuu wa neno la Mungu kwa kusema kwamba neno hili linanguvu na ukali kama upanga mkali. Na mbele ya neno hili, kila kitu kinakuwa wazi-hakuna kinachofichika.

Huu ndio ukuu wa Mungu ndugu zangu, kwake yeye hatuwezi kuficha kitu, na yeye hapendi dhambi. Shukrani kwa Yesu. Yeye ndiye aliyekuhani mwenye kutuombea mbele ya Mungu. Kweli tukienda mbele ya Mungu bila Yesu kutuombea, hakika nafasi yetu ni finyu. Yesu yupo. Tumwangukie nasi tutaweza kumfikia Baba. Tusiache kumwamini Yesu hata siku moja.

Somo letu la injili linatuhimiza kuanzisha urafiki na Yesu ili tupate okolewa. Leo Lawi anaanzisha naye urafiki na hakika anafaidi sana. Anapatwa kufundishwa juu ya dhambi zake na kama tutaendelea kusoma hii sehemu ya injili, tutagundua kwamba Lawi alichomwa na Yesu na hata kudiriki kurudisha kile alichodhulumu. Huyu ndiye Yesu kuhani wetu. Hakika anatupenda sana. Anapokutana na watoza ushuru na makahaba, hawafukuzi, anawaalika, kwani Yesu anajua hali yao lakini taratibu wao wenyewe wanaanza kubadilika na kuacha maisha yao ya zamani kama wanavyofanya akina Mathayo (Lawi) leo.

Sisi nasi tuwe na upendo kwa wenzetu hata wale waliotukosea. Tutambue kwamba Bado ni viumbe vya Mungu na tuwasaidie kumrudia Mungu.

Tusitangaze dhambi ya yeyote, mlete kwa Yesu naye atabadilishwa kama Lawi anavyobadilishwa leo. Tusiogope kukiri makosa yetu mbele ya Yesu, yeye anatufahamu sisi mno, tuwe wazi kwake atufanye upya.

Maoni


Ingia utoe maoni