Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Ijumaa, Januari 15, 2021

Ijumaa, Januari 15, 2020,
Juma la 1 la Mwaka wa Kanisa

Ebr 4: 1-5, 11;
Zab 77: 3-4, 6-8;
Mk 2: 1-12

WAKATI MUNGU AKIWA KIMYA

Karibuni ndugu zangu kwa tafakari ya neno la Mungu asubuhi ya leo katika adhimisho la Misa Takatifu. Leo neno la Bwana katika Zaburi yetu ya wimbo wa katikati, mzaburi anasisitiza kwamba tusiyasahau matendo ya Mwenyezi Mungu kamwe.

Tusisahau na maajabu yake, yote. Yafaa yasimuliwe kwa vizazi vijavyo na kamwe tusiige ukaidi kama ule walionesha baadhi ya wazee wa taifa la Israeli. Ukaidi wao uliomfanya Mungu asiheshimike na vizazi vijavyo.

Somo letu la kwanza linatukumbusha juu ya uwepo wa pumziko lililoandaliwa na Bwana-na kwenye kulipata pumziko hili, bado hatujachelewa. Tunaaswa kwamba ikiwa tutakumbatia moyo wa ukaidi, hakika tutashindwa kulipata pumziko hili. Wazee wa taifa la Israeli walipoonyesha ukaidi, walishindwa kufika katika nchi ya ahadi na kupata pumziko. Waliishia kufa jangwani kwa sababu ya kuifanya migumu mioyo yao.

Sisi tukija kwa Bwana tusifanye migumu mioyo yetu, tukija kwa Bwana lazima tuyeyuke kama nta mbele ya moto, lazima tuanguke kifudifudi tukitambua kwamba hakuna kama yeye. Ukaidi wetu na majivuno vitatukosesha mengi.

Katika injili yetu, tunakutana na waandishi wakiifanya migumu mioyo yao, hawataki kuifungua na kuona muujiza uliofanywa na Yesu. Wanakataa pia kuona imani na maumivu ya mgonjwa. Wanaishia kutafuta makosa toka kwa Yesu. Hapa waliifanya migumu mioyo yao na hakika wasingaliweza kumwamini au kupewa pumziko na Bwana Yesu.

Sisi ndugu zangu tusioneshe ukaidi mbele ya Mwenyezi Mungu. Wengi tunalisubiri hili pumziko litutulize. Ulimwenguni tunateseka lakini tunategemea kwamba ipo siku tutaokolewa na Bwana Yesu na kupewa hilo pumziko ikiwa tutaendelea kuilainisha mioyo yetu.

Maoni


Ingia utoe maoni