Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatano, Januari 13, 2021

Jumatano, Januari 13, 2021,
Juma la 1 la Mwaka wa Kanisa

Ebr. 2:14 – 18
Mk. 1:29-39


Ndugu zangu katika Kristo karibuni kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo neno la Bwana katika injili yetu tunakutana na Yesu akitenda miujiza mingi, watu wakifurahia. Lakini anatambua kwamba ni wengi walio na uhitaji na hivyo anakataa kumilikiwa na kundi moja tu na kwenda sehemu nyingine kuwahubiria wengine habari njema. Anatambua kwamba wahitaji ni wengi na hivyo anaamua kuwafuata.

Injili hii iwe kwetu fundisho kubwa ndugu zangu. Wengi wetu tunatabia ya kujishikiza kwa watu wachache tu na kufanya nao kazi. Mwisho wa siku ni wao tu huishia kufaidi na kuwatelekeza wengine. Tupambane na kishawishi cha kutaka kumilikiwa na watu fulani tu au watu wa eneo fulani tu. Wahitaji ni wengi. Tutoke tuende mbali zaidi.

Somo hili litusaidie pia sisi sote tulio na vyeo au madaraka au ujuzi mbalimbali. Tushirikishane ujuzi huu na watu wa aina zote. Ofisi zetu ziwapokee watu wa aina zote. Matajiri, maskini, makabila na dini zote. Kristo hakubagua. Tusikubali kuvimbishwa vichwa na sifa chache za watu na kutekwa kirahisi.

Katika somo la kwanza, tunaelezwa juu ya ubora wa Kristo kama kuhani mkuu. Yeye ni kuhani bora anayeweza kuchukuliana nasi kwani alikubali kuchukua hali yetu-anatambua mateso yetu na udhaifu wetu na hivyo aweza kutuombea vyema machoni pa Baba. Hili tunaliona vyema katika injili ambapo anatambua maumivu ya wanadamu na kuwaponya.

Nasi ndugu zangu tusiogope kumlilia Yesu. Yeye ajua hali yetu yote, ajua ugumu tunaopitia. Hakuna anayeielewa hali ya mwanadamu kama Yesu. Hivyo yeye ndiye wa kuelezwa shida. Tuwapelekee pia wengine Yesu ili nao wapate kusikilizwa shida zao. Kama mama mkwe wa Simon asingaliletewa Yesu, hakika asingalipona. Sisi tuwapelekee wengine Yesu. Tusiwapeleke kwenye ushirikina. Tuwapelekee Yesu. Hakika maisha yao yatakuwa bora zaidi.

Maoni


Ingia utoe maoni