Jumapili. 24 Novemba. 2024

Tafakari

Jumanne, Januari 05, 2021

Januari 5, 2021.
------------------
Jumanne, baada ya Epifania

1 Yn 4: 7-10;
Zab 72: 1-4, 7-8;
Mk 6: 34-44.

KUTAMANI UTAKATIFU!

Ndugu zangu wapendwa karibuni kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Yesu katika injili anakutana na makutano ya watu, wanaotangatanga na kuangalia kama kondoo wasio na mchungaji.

Kondoo asiye na mchungaji mara nyingi huishia kula takataka kwa kukosa mchungaji wa kuwaongoza. Halafu hajui aendako na mara nyingi hupotea kirahisi au kuliwa na wanyama wakali.

Yesu aliwaona makutano wakiwa katika hali hii. Walikabiliwa na vitu kama magonjwa, njaa, ukosefu wa imani na maarifa. Yote haya yangewasababishia kuishia kutekwa na ushirikina, uregevu, na imani potofu. Lakini Yesu aliamua kuingilia kati na kuwalisha neno na kuwaongoza.

Sisi kila mara tupo na kondoo wasio na mchungaji. Tupo na mayatima lakini wanaishia kuwa chokoraa mtaani, wapo wagonjwa waliokata tamaa na kuishia kwenye ushirikina. Yote haya yanatuhimiza tujitolee, tuchukue nafasi ya uchungaji. Tukikutana na yatima waliotelekezwa tuchukue nafasi ya uchungaji. Tukikutana na familia iliyojaa uregevu basi tuchukue nafasi ya uchungaji. Imani yetu yahimiza tujitolee zaidi.
Tuongeze majitoleo. Bila majitoleo ama kweli injili ya Bwana itashindwa kusonga mbele.

Somo la kwanza linatusisitizia tuwe na upendo. Upendo wadai majitoleo. Yesu alijitolea na kwa majitoleo hayo, sisi sote tumeweza kupewa uzima. Sisi tujitolee ili na wenzetu wapate uzima. Wengi wanapoteza uhai kutokana na kukosekana kwa wanaojitolea. Tuiokoe dunia kwa kuongeza idadi ya wanaojitolea. Tuanze sasa, kwa majitoleo yetu wenyewe dunia itapata baraka na nafuu.
Tumsifu Yesu Kristo.

Maoni


Ingia utoe maoni