Jumatatu, Januari 04, 2021
Januari 4, 2021.
------------------
Jumatatu, baada ya Epifania
1Yoh. 3:22-4:6
Mt. 4:12-17, 23-25
Karibuni ndugu zangu katika dhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo tunachojifunza katika masomo yetu ni kwamba tamaa hukwamisha utume wa Bwana.
Leo neno la Bwana katika somo la injili, tunamkuta Yesu akianza kazi yake ya umasiha. Anajitokeza mtaani na moja kwa moja anakwenda kwa wale wanaoteseka, anahubiri habari njema huko na kuponya na kutoa matumaini. Injili hii inatuambia kwamba Yesu anaanza utume wake katika Galilaya ya mataifa, eneo lililodharaulika, lenye watu wengi wasio na mchungaji. Yesu anaanzia hapo. Ndipo atakachopochagua na mitume wake na kufanya miujiza mingi.
Eneo hili lilikuwa na njaa ya kuhubiriwa habari njema. Yesu aliamua kwenda kwenye eneo la watu wa chini. Sisi nasi tutambue kwamba utume wa kanisa lazima ulenge watu wa chini, usiwatekeleze, uwapatie nafasi. Lakini cha ajabu kipindi chetu ni tofauti. Wengi tunangangania utume kwa sehemu za watu wa juu. Sehemu za matajiri zina watumishi wengi sana kiasi kwamba wengine hawahitajiki. Sehemu za watu wa chini hakuna kitu. Hata watu wa chini wenyewe wanaacha kufanya utume kwenye yale maeneo yao wanakwenda ati kule kwa watu wa juu. Tuache kuweka maslahi binafsi mbele.
Yesu hakuweka maslahi binafsi mbele. Tuone huruma ni kwa namna gani kuendekeza kwetu tamaa kumewaacha maskini wengi bila kulisikia neno la Mungu na kuishia kuishi tu hivihivi-namna gani tamaa zangu zinavyorudisha utume wa Kristo nyuma. Kazi ya Kristo isifanywe kwa tamaa bali kwa moyo safi kabisa.
Somo la kwanza linakumbushia juu ya uwepo wa manabii wengi wa uongo. Wengi tunakuwa manabii wa uongo kwa sababu ya tamaa na kuigeuza injili ya Kristo. Tunaigeuza injili ya Kristo na kuifanya iseme kile tunachotaka kusikia au kuona ambacho kinaendana na maslahi yetu na mategemeo yetu.
Mahali pengi injili ya Kristo inatafsiriwa kiajabu. Yote haya ni kutokana na kutanguliza tamaa mbele. Tutambue kwamba tamaa mbele mauti nyuma. Hatutabarikiwa kwa kuigeuza geuza injili ya Kristo kiajabu ajabu hivi. Ni lazima tufikie mahali tuwe wakweli na kuipatia injili hii tafsiri sahihi. Tumsifu Yesu Kristo.
Maoni
Ingia utoe maoni