Jumatano, Disemba 09, 2020
Desemba 9, 2020.
JUMATANO, JUMA LA 2 LA MAJILIO
Somo la 1: Isa 40: 25-31 Mungu anajifunua mwenyewe kama Mwenyezi, anayefahamu yote, na bado anawajali watoto wake, wale wote wanao mtumaini hawata tikisika wala kuwa na hofu.
Wimbo wa katikati: Zab 102: 1-4, 8, 10 Moyo wangu wamtukuza Bwana kwani ni yeye mwenyewe anayesamehe udhaifu wetu, anaye okoa maisha yetu kutoka katika kaburi, anaye kuvika kwa upendo na huruma.
Injili: Mt 11: 28-30 Yesu anatualika sote tumuendee, tuchukue nira yake na kujifunza kwake, kwani ni mpole na mnyenyekevu wa moyo.
------------------------------------------------
TUKABIDHI MIZIGO YETU TUPATE PUMZIKO KWA YESU!
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo na leo masomo yetu yanaongozwa na maada ya kuwa, Bwana ni Mwenye Uwezo Mkubwa, Mtumainie.
Somo la kwanza wana wa Israeli wapo nchini Babuloni na wanashangazwa na sifa anazopewa huyu Marduku, mungu wa Babuloni na watu wake. Wao walimtangaza Marduku kama Mkuu, aliyewawezesha hata kuwakamata mateka wana wa Israeli. Hivyo, walimtangaza Marduku kuwa mkuu zaidi ya Bwana Mungu wa Israeli. Wana wa Israeli waliposikia habari hizo-na kuangalia maendeleo ya wana wa Babuloni, waliogopa, wakanywea, wakidiriki hata kukosa imani.
Leo Isaya anawaeleza kwamba Mtumainieni Mungu, Mungu wetu ni mwenye uwezo mkuu, yeye ndiye aliyeifanya dunia na kuiweka mahali pake, ni yeye tu awezaye hili. Hakuna zaidi yake.
Sisi nasi tunamhitaji Isaya mwingine aje atutie nguvu. Wengi wetu tumekata tamaa, hatuoni tena kwamba Mungu ana nguvu tena, tukitishiwa na ushirikina kidogo tu tayari tunaogopa ajabu, au ukitishiwa na mwenye pesa kidogo tu, tayari unaogopa na kukosa amani, au msichana akiona umri unapita bila ya yeye kuolewa yaani anaogopa anakuwa tayari hata kubadili dini ajiuze tu kwa mtu wa dini tofauti. Mwingine akiishiwa pesa hapo mfukoni ataogopa ajabu.
Sisi ndugu hatupaswi kuogopa hivyo, Mungu wetu ana nguvu za ajabu, sio wa kutishiwa na vitu vidogo kama hivi. Tunafanya haya kwa sababu hatuujui ukuu wa nguvu za Mwenyezi Mungu. Sisi tumtegemee Bwana, hakika tusiwe watu wa kutishiwa na mambo madogo na kukosa amani.
Somo la injili tunaalikwa tupeleke masumbuko yetu kwa Bwana. Haya ni maneno yaliyojaa furaha kubwa. Ni wangapi wanaofarijiwa na Bwana? Lakini nakueleza, mimi kwenye tafakari zangu naona kwamba kama ingekuwa tumekwishalikumbatia fundisho hili, tusingalisumbuka namna hii ndugu zangu. Tubadilike. Ulimwenguni tunahitaji kufarijiwa na Bwana na bila hili hatutaweza kusonga mbele.
Kuna majanga na mapito mengi mno. Siku itakuja ambapo utajisikia mambo hayaendi kabisa, unaona maisha hayana maana, hata ulichojitahidi kulima au kujiwekea akiba hakina maana. Kweli hapa ndipo utakapoona umuhimu wa Bwana. Bila Bwana mwanadamu hawezi kusonga mbele. Asante ee Bwana kwa kukubali kuwa nasi.
Maoni
Ingia utoe maoni