Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Alhamisi, Novemba 26, 2020

Alhamisi, Novemba 26, 2020,
Juma la 34 la Mwaka wa Kanisa


Ufu 18:1-2, 21-23; 19:1-3, 9;
Zab 99:2-5;
Lk 21:20-28


UAMINIFU WA MUNGU!

Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo neno la Bwana katika somo la kwanza Yohane anaeleza juu ya kuteketea kwa yule kahaba mkuu, aliyewahi kuwa maarufu na kujiona kutawala dunia nzima. Anaaibishwa na kibao kinawageukia wale aliowatesa; wakati wanaanza kufurahia utawala wa Mwenyezi Mungu, yeye atakaa katika shida.

Somo hili linatoa somo kwetu sisi hasa sisi tunaonekana na baadhi ya watu kuwa ni vijana, maarufu, wababe, wenye misuli na waheshimiwa. Heshima hizi au ujana wetu au misuli yetu hazitasalia nasi kwa miaka yote. Upo wakati nasi tutakuwa wazee, watoto tuliowanyanyasa watakuwa na nguvu zaidi yetu na kila tutakapotamani kuwa na nguvu kama zamani, kamwe hatutafanikiwa tena. Hivyo duniani tuishi kipole. Tusimnyanyase yeyote hata akiwa maskini, mtoto au kichaa. Nyakati zinabadilika pia.

Kati yetu kuna waliowahi kuwa maarufu sana, tukaponda ujana kweli lakini kwa sasa hivi tumechakaa kabisa na tunashindwa kuamini kwamba upo wakati tuliowahi kuwa vijana na sisi. Tuishi kipole, tutumie misuli yetu, ujana wetu, usichana wetu vyema na tumtukuze nao Mungu. Haya yote yana mwisho.

Katika injili Yesu anaendeleza tena juu ya ukweli kwamba mambo ya dunia yana mwisho kwa kueleza juu ya shida atakazopata Yesusalemu. Huu ulikuwa mji maarufu, ulijiona kufahamu mengi, kuwa na viongozi hodari, kuwa na hekalu la Mungu, kuwa na makaburi ya wakuu kama Daudi. Walifikiri mji huu hautakaa ushindwe.

Lakini mwishowe walijishangaa kuona ukianguka na wengi kuuangamia. Haya yatatokea na kwetu endapo tutaishia kujisifia na kujitangaza kuwa watakatifu bila ya sisi kufanya bidii kila siku. Anayejitangazatangaza kwamba yeye ni mteule wa Bwana na kujidai kwamba atalindwa tu na Mungu bila ya kuongeza bidii na kumwomba kila siku ulinzi huanguka kihivihivi na kukamatwa na shetani.

Shetani huwakamata kirahisi walio na majivuno; wanaojiita kwamba wameokoka na kumbe bado wapo katika udhaifu na hawakazani kumwomba Mungu awaokoe. Sisi tupunguze majivuno na kumwomba Mungu kama hitaji letu na hapa tutaweza kumpokea Mungu siku ya Mwisho na yeye kutuokoa.

Maoni


Ingia utoe maoni