Jumatano, Novemba 25, 2020
Jumatano, Novemba 25, 2020,
Juma la 34 la Mwaka wa Kanisa
Ufu 15:1-4;
Zab 97:1-3, 7-9;
Lk 21:12-19
UVUMILIVU UTAOKOA MAISHA YENU!
Ndugu zangu karibuni kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo.
Kwa uvumilivu wenu, mtayaokoa maisha yenu. Haya ni maneno ya injili ya Yesu leo anapotueleza juu ya ujio wa ujio wa siku za mwisho na vishawishi viwezavyo kutufanya tupoteze imani yetu.
Anatueleza kwamba njia ya kufikia mbinguni sio rahisi, yahitaji uvumilivu mkubwa. Unapotaka kumtumikia Bwana, shetani anakuja pia karibu akiwa na lengo la kukuzuia ili Bwana asipate mtumishi. Atajitahidi kuleta kila aina ya vishawishi na mateso.
Enzi za mitume, mateso yaliyoletwa na shetani ni kutengwa na ndugu zako wa damu kwa sababu ya mtu kuiacha dini yake ya asili hivyo unatengwa na kuchukiwa na wajomba, kaka, dada na wazazi na pengine wanakufukuza hata nyumbani. Pia kulitokea watawala waliowachukia wakristo na kuwatesa wakitaka waikane imani yao.
Hizi zote ni njia alizotumia shetani kuiangusha injili. Siku hizi kwa sababu ya uwepo wa utawala wa sheria na uteteaji wa haki za kibinadamu shetani amegeuza vishawishi vya kutufanya tusimtumikie Kristo na hivyo tuikose mbingu. Hivi ni vishawishi kama kuanzishwa kwa kumbi nyingi za starehe au ushabikiaji wa michezo mbalimbali inayotufanya hata tukose kanisani-mfano kipindi cha kombe la dunia wengi tunakosa kanisani pengine tukitaka kuangalia mechi.
Pia kutumia muda mwingi katika simu. Njia zote hizi zaweza kutufanya tushindwe kumtumikia Mungu.
Kwenye somo la kwanza tunaambiwa kwamba ni waliopata ushindi ni wale waliopitia katika dhiki iliyokuu na hawa wanapata nafasi ya kumshangilia Mungu kwa matendo yake makuu ya kuwakomboa. Sisi tumshukuru Mungu kwani kila siku anatupigania na kutupatia pumzi, na amani, na kazi na marafiki wazuri wanaotuzunguka. Tuanze kumtukuza Mungu kwa wimbo kama huu kila kila mara.
Tuache kumpatia shetani sifa kila kukicha kwa kuwaza au kuongea maneno machafu, kuangalia picha mbaya au vichekesho vya dhambi. Tujitahidi basi hata kuangalia filamu za Yesu, Bikira Maria na watakatifu na kusoma Biblia kuliko kuongea maneno machafu kila siku na kumshushia Mungu utukufu wake. Sisi tumpatie Mwenyezi Mungu utukufu wake kwani anastahili kama tulivyoadhimisha jumapili ya Kristo Mfalme.
Maoni
Ingia utoe maoni