Jumapili, Novemba 22, 2020
Jumapili, Novemba 22, 2020
Dominika ya 34 ya Mwaka
Sherehe ya Yesu Kristo Mfalme
Eze 34:11-12.115-17
Zab 23:1-3.5-6
1Kor 15:20-26.28;
Mt 25:31-46
AGANO JIPYA NA MFALME
Sherehe ya Kristo Mlame ni sherehe ya Agano na Mungu. Mara nyingi tunavyosikia Agano tunafikiria kuhusu Wayahudi walivyokuwa na Agano na Mungu. Lakini maanDiko yanaitwa “Agano Jipya” na yanaonesha maagano yetu mapya na Bwana Mungu. Na sehemu tulipofanya Agano hili ni siku ya Ubatizo. Tulibatizwa ndani ya Kristo na ndani ya Agano jipya naye.
Somo la kwanza linatoka katika kitabu cha nabii Ezekiel na linamuongelea Mungu kama Mchungaji. “waliopotea nitawatafuta, waliopotea nitawarudisha, walio umia nitawafunga majeraha….” Mara nyingi maneno makali katika Agano la Kale yanawaogopesha watu siku hizi. Nabii Ezekieli akiongea kwa jina la Mungu anatuambia “walio nona na wenye nguvu nitawangamiza”. Hii haina maana kwamba ni Mungu anataka kuondoa na kuwaangamiza baadhi yetu. Bali ni kupigwa msasa na Mungu nakutaka kumfanya mtu kuwa kiumbe kipya cha Kimungu. Wale wenye nguvu na kunona mara nyingi huishi katika hali ya kujidanganya na kujiona watawala lakini nguvu kamili ni Yesu. Hali ya kujidanganya inabidi iharibiwe au kupigwa msasa na kurudishwa katika mstari wa kumfuata Yesu aliye mfalme wa kweli. Sisi wote tunapaswa kujiweka kwake hakuna aliye mkuu zaidi. Tupo ndani ya Agano na Mungu na Mfalme wetu ni Kristo.
Somo la Pili linatoka katika barua ya kwanza ya Mtume Paulo kwa Wakorintho inaongelea lengo kuu la kuishi katika maisha haya ni Kristo na kushiriki ufufuko wake. Kila kitu kinapaswa kuwa kadiri ya mapenzi ya Mungu na kuishi kadiri ya mapenzi hayo. Hivyo, kwanini tuna uhuru? Ili tuweze kujitoa wenyewe kwa Kristo na kumfuata yeye daima. Mungu ana huruma sana juu yetu na hata anatuvumilia kufanya kazi na sisi, hata kama hiyo kazi ni kwa ajili ya kutuunda upya kwakuharibu yale yanayopinga mapenzi yake na kutupangia mipango mipya.
Katika somo la Inili kutoka katika Injili ya Mathayo, anatuambia kwamba kadiri tunavyo watendea hawa walio wadogo tunamtendea Kristo mwenyewe. Hili tunalifahamu kwa akili zetu lakini mara nyingi hatulifanyi hili katika maisha yetu ya kila siku. Tunapewa changamoto ya kumuona Yesu katika kila sura ya kila mtu, hasa wale wanao tuudhi na kutufanyia kila lilolo baya na kujikuta sisi tunachukia kila siku. Ndio maana Yesu anatuambia daima kwamba tuwapende maadui wetu. Ni rahisi kumpenda rafiki.
Hadithi moja ya Ireland, inaeleza wakati ambapo nchi ya Ireland ilitawaliwa na wafalme. Mflame aliyekuwa anatawala hakuwa na mtoto wa kuirithi enzi yake. Hivyo, aliwatuma wajumbe wake kutangaza ujumbe wake katika kila mji na kijiji cha utawala wake. Aliwaalika vijana waliohitimu kwa mkutano na Mfalme. Mfalme alihitaji sifa mbili: mtu lazima awe na upendo wa kina kwa Mungu na kwa jirani yake.
Kijana mmoja alisikia tangazo hilo. Kwa hakika alikuwa na upendo wa dhati wa Mungu na kwa jirani. Lakini, alikuwa ni maskini sana, na hakuwa na mavazi ya adabu ya kuvaa katika mkutano na hakuwa na fedha za kununulia mahitaji muhimu kwa ajili ya safari ndefu kwenda kwenye ngome ya Mfalme. Aliamua kwenda kuomba nguo na mahitaji aliyotaka. Kila kitu kilipokuwa tayari, alianza safari yake. Baada ya mwezi mmoja wa safari, alifika karibu na ngome ya Mfalme, alimwona maskini mwombaji akikaa kando ya barabara. Mwombaji alinyanyua mikono yake juu akiomba msaada. “nina njaa na kujisikia baridi?” alisema kwa sauti ya kutetema, Je! unaweza kunipa kitu chochote nipate kula na nguo kuvaa? Kijana yule alivutwa sana na mwombaji. Alizitoa nguo zake za nje na kubadilishana na nguo za mwombaji zilizochakaa na kuchanika. Pia alimpatia mwombaji yule mahitaji aliyokuwa amebeba kwa ajili ya safari. Hii hairidhishi sana alitembea na nguo zilizochakaa kwenda kwenye ngome ya Mfalme. Alipofika kwenye ngome ya Mfalme, askari alimchukua kumpeleka eneo la wageni. Baada ya muda mrefu aliongozwa kwenda kumwona Mfalme. Aliinama kifudifudi mbele ya enzi ya Mfalme na aliponyanyua kichwa juu hakuweza kuamini macho yake. Alipomuona mfalme alimwambia: “Wewe ulikuwa ni mwombaji kando ya barabara!” Hakika ni kweli” alisema mfalme, “Nimetaka kujua zaidi kama hakika wampenda Mungu na jirani.”
Hadithi hii hakika inalingana na liturujia ya leo. Mfalme wetu ni Mfalme mwenye Upendo. Anatupenda sisi bila kikomo kwamba yeye alikuwa tayari kutoa utukufu wake kutuokoa kutoka katika utumwa wetu wa dhambi. Ukweli alishuhudia Upendo. Je, sisi tunaweza kusikiliza sauti ya upendo wake
Hivyo kama Kristo Mfalme ni Mfalme wetu, tunapaswa kuishi agano letu naye. Tunapaswa kutembea kwa unyenyekevu naye na kumwamini katika kuwapenda wenzetu na upendo wa Mungu udhihirike katika maisha yetu. Sherehe hii sio tu kumwangalia Bwana wetu kama Mfalme, hapana, nikutazama juu ya Agano letu na huyu Mfalme kama tunatembea katika mapenzi ya Mfalme au tumechukua ule ufalme wake na kujifanya sisi Wafalme? Yeye anataka kutupenda sisi daima kwasababu na sisi tunapenda wote daima.
Tafakari leo, juu ya kumpokea Kristo kama Mfalme. Je, yeye anaongoza maisha yako katika kila nyanja? Je, unamruhusu yeye awe na uwezo wa kila kitu katika maisha yako? Kama hili likifanyika kwa uhuru kamili ufalme wa Mungu unaanzishwa katika maisha yako. Mwache yeye atawale ili wewe uweze kuongoka. Na kwa njia yako watu waweze kumfahamu kama mfalme wa wote. Kama wajumbe wa Kristo Mfalme tutambue kwamba sisi tutahukumiwa kwa njia ya sheria ya upendo pekee. Hivyo tujikabidhi katika ufalme wake wa upendo.
Sala:
Bwana, wewe ni mfalme wa ulimwengu. Wewe ni Bwana wa wote. Njoo utawale maisha yangu na ufanye moyo wangu kuwa sehemu yako ya kuishi. Bwana, njoo, ufanye ulimwengu wetu kuwa sehemu yako ya amani na haki. Ufalme wako ufike! Yesu nakuamini wewe.
Amina.
Maoni
Ingia utoe maoni